JAMII,WADAU TUSHIRIKIANE KUSAIDIA WENYE MAHITAJI YA VIUNGO BANDIA - RC KUNENGE
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani ,Abubakari Kunenge amewataka wadau na wale wenye uwezo wa kusaidia watu wenye ulemavu wenye mahitaji ya viungo bandia,kuwawezesha ili waweze kuendelea na shughuli zao.
Aliyasema hayo Mjini Kibaha wakati wa ufunguzi wa Desire Charitable Hospital and Rehabilitation Centre (DCHRC) kilichopo Wilayani Kibaha.
Alisema ,kituo hicho cha afya ambacho kinatengeneza viungo bandia na kutoa matibabu mbalimbali kitasaidia wenye mahitaji hayo hasa ikizingatiwa kuwa mkoa wa Pwani ni mkoa wa mkakati wa viwanda hivyo huduma za afya zitahitajika kwa kiasi kikubwa.
"Toeni taarifa ili watu wenye uwezo waweze kuwanunulia watu viungo bandia kwani kuna watu wenye moyo wa huruma watasaidia wengine ili kuwarejeshea faraja watu wenye matatizo ya viungo,"alisema Kunenge.
Aidha anaishukuru serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa mkoa huo ili kuboresha huduma za afya.
"Baadhi ya miradi Mkoa iliyopata fungu hilo ni pamoja na kiasi cha shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi vituo vya afya 10, bilioni 2.7 kwa ajili ya miradi ya covid-19, ujenzi wa vyumba dharura ICU kwenye Wilaya tano za Mafia, Kibiti, Rufiji, Bagamoyo na Kisarawe.
Alibainisha kuwa utoaji huduma bora za afya kwa wagonjwa ni ibada kwani huduma hizo zinahitaji ucha mungu kwani wanahudumia wagonjwa kama familia zao,amezitala Tanroads na Tarura kurekebisha barabara inayoelekea kwenye kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake mtendaji mkuu wa kituo hicho cha afya ,Stella Kitali alifafanua wamejikita kutengeneza viungo bandia na kutibu mifupa .
Alibainisha,watatoa huduma asilimia 25 ya wagonjwa wasioweza kulipia matibabu, watatibiwa kwa gharama nafuu au bure kabisa kwa kipindi cha miaka mitano.
Kituo hicho kilianza kutoa huduma April mwaka huu na imeajiri wafanyakazi 20 na mradi wa ujenzi huo umesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) na ukikamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.
No comments: