BENKI YA NMB YACHANGIA MILIONI 120/= KUFANIKISHA MAANDALIZI NA KUFANYIKA MKUTANO MKUU WA 36 WA ALAT MKOANI MBEYA
Benki ya NMB imechangia kiasi cha shilingi milioni 120 kufanikisha maandalizi na kufanyika kwa mkutano mkuu wa 36 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) wa mwaka huu unaonza leo jijini Mbeya.
Akikabidhi mfano wa hundi ya mchango huo kudhamini shughuli hiyo ya siku tatu, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema wataendelea kushirikiana na ALAT kulihudumia Taifa huku wakiendeleza mahusiano mema baina yao.
“Uhusiano kati yetu na ALAT ni wa muda mrefu na umekua wa manufaa makubwa kwa pande zote mbili. Kwa miaka mingi tumekuwa na mashirikiano na ALAT katika ngazi zote kuanzia halmashauri hadi ngazi ya Taifa. Katika
kuendelea kuimarisha mahusiano yetu, kama benki tumeona ni vyema tushiriki katika kufanikisha mkutano huu utakaoanza leo kwa kuchangia kiasi cha shilingi milioni 120,” alisema Ruth.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa mkutano huo ambao kauli mbiu yake, inasisitiza kuongeza tija katika ukusanyaji na matumizi ya mapato katika halmashauri kama msingi bora wa maendeleo endelevu ya wananchi.
Benki ya NMB inatambua kazi kubwa inayofanywa na ALAT chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa ALAT Taifa - Bwana Murshid Ngeze na Katibu Mkuu wake - Ndugu Elirehema Kaaya, katika kusimamia na kutekeleza malengo yake.
Uongozi wa ALAT ukiongozwa na Katibu Mkuu wake ndugu Elirehema Moses Kaaya, uliishukuru Benki ya NMB kwa ajili ya udhamini huo, huku ukisisitiza kuwa benki hiyo imekuwa sio tu mshiriki mwema wa ALAT, lakini pia kwa serikali kwa ujumla kwani wamekuwa wakishiriki katika shuguli zake nyingi lakini hata katika kuchangia shuguli za kimaendeleo, hususani katika sekta ya elimu na afya.
NMB pia ilidhamini Mkutano Mkuu wa ALAT wa mwaka jana uliofanyika Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 500 kutoka halmashauri 185 za majiji, wilaya na manispaa kote nchini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB - Bi. Ruth Zaipuna akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 120 Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) Mheshimiwa Sima Constatine Sima, ikiwa ni udhamini wa benki hiyo katika mkutano mkuu wa Jumuiya hiyo, unaotarajiwa kifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango leo na kumalizika siku ya Jumatano ya tarehe 14 jijini Mbeya.
No comments: