Balozi Dkt . Chana azindua Bodi ya Wakurugenzi NCAA

 


Na mwandisi wa NCAA, Arusha.


Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) leo tarehe 28 Septemba, 2022 amezindua bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo iliteuliwa hivi karibuni.

Katika tukio hilo Mhe. Waziri Chana ameielekeza Bodi hiyo kutekeleza mkakati wa serikali wa kuboresha miundimbinu ya utalii, kuimarisha shughuli za Uhifadhi na kuongeza jitihada za kuongeza idadi ya watalii nchini kufikia watalii milioni 5 mwaka 2025.

Pia ameielekeza Bodi hiyo kwa kushirikiana na menejimenti ya NCAA kuendelea kubuni mazao mapya ya utalii ili kuvutia wageni wanaotembelea Nchi yetu pamoja na kupanga mikakati ya kutangaza na kukuza utalii wa vivutio vilivyoko Ngorongoro.

“Sambamba na kuboresha miundombinu ya Utalii pia tuendelee kuhifadhi, kulinda maliasili lakini kubuni mazao mapya ya utalii yatakayosaidia idadi ya wageni kuongezeka kufikia idadi ya milioni 5 mwaka 2025 kama tunavyoelekezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi” Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Waziri wa Maliasili na Utalii.

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo ameeleza kuwa Bodi anayoiongoza imejipanga kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kusimamia shughuli za Uhifadhi, Utalii, Maendeleo ya jamii ili kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinahifadhiwa, kutunzwa na kuongeza tija ili ziwe na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

“Tumeona jitihada mbalimbali za serikali kutangaza utalii hasa kupitia kampeni ya Mhe. Rais ya Tanzania The Royal Tour na kupelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini hasa baada ya janga la UVIKO-19 lililotikisa dunia.

"Bodi ya Wakurugenzi tunaahidi kuendeleza jitihada hizi kuhakikisha tunafikia idadi ya watalii milioni tano (5) kwa mwaka 2025 kama malengo ya Wizara yanavyosema” Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, NCAA.

Jenerali Mstaafu Mabeyo ameongeza kuwa Bodi anayoiongoza itahakikisha Mamlaka inabuni mazao mapya ya utalii, kuboresha huduma kwa watalii na kutumia mikakati madhubuti ya kutangaza vivutio ili kuvutia wageni wengi zaidi na kuongeza mapato kwa nchi.

Naibu Katibu Mkuu - Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Juma Mkomi ameeleza kuwa kutokana na jitihada na mikakati mbalimbali ya serikali ya kutangaza utalii hasa kupitia kampeni ya Mhe. Rais ya Tanzania, The Royal Tour idadi ya wageni imeendelea kuongezeka na kufikia 425,386 na mapato kuongezeka na kufikia TZS. Bilioni 91.1 mwaka 2021/22.

Amefafanua kuwa Serikali inaamini idadi hii ya watalii na mapato yataongezeka maradufu kwa mwaka 2022/23 kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Freddy Manongi, Hifadhi ya Ngorongoro ni eneo pekee Afrika lenye hadhi tatu kutoka Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (UNESCO).

Amezitaja hadhi hizo kuwa ni Hadhi hizo ni pamoja na Eneo la Urithi wa Dunia Mchanganyiko (Mixed World Heritage Site), Eneo la Hifadhi Bayoanuai (Man and Biosphere Reserve) na Eneo la Utalii wa Jiolojia (UNESCO Global Geopark), Kutokana na hadhi hizi za kimataifa, eneo hili limekua likivutia wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali duniani ambao huchangia mapato makubwa kwa serikali na wananchi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) akikata utepe wa Nyaraka za Sheria mbalimbali kama kitendea kazi kwa ajili ya kumkabidhi Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo leo Septemba 28,2022 jijini Arusha wakati akizindua bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliyoteuliwa hivi karibuni,kulia anaeshuhudia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) akimkabidhi Nyaraka za Sheria mbalimbali kama kitendea kazi Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa NCAA Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo leo Septemba 28,2022 jijini Arusha wakati akizindua bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo iliyoteuliwa hivi karibuni
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa NCAA Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo akizungumza jambo mbele ya Wageni waalikwa wa hafla hiyo leo Septemba 28,2022 jijini Arusha mara baada ya kuzinduliwa bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo iliyoteuliwa hivi karibuni




No comments: