NI WAJIBU WETU KUMLINDA MTOTO DHIDI YA UDHALILISHAJI - MAMA ZAINAB

Mwenyekiti wa Taasisi ya Nuru Zanzibar, ambayepia ni Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, akizungumza na wazazi na Watoto kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Mkoani Pemba, katika ziara yake ya kuwasalimia, kuwafariji na kuwagawia misaada wananchi mbali mbali wakiwemo watoto yatima na wenye mazingira magumu, kikao kilichofanyika Skuli ya Mwambe Mkoa wa Kusini Pemba leo Agosti 21, 2022. Kushoto kwa Mama Zainab ni Bw. Khatib Juma Mjaja (Mkuu wa Wilaya ya Mkoani-Pemba)Mwenyekiti wa Taasisi ya Nuru Zanzibar, ambayepia ni Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib,akisalimiana na Mzee Yusuf Othman wa Mwambe Mkoa wa Kusini Pemba, katika ziara yake ya kuwasalimia, kuwafariji na kuwagawia misaada wananchi mbali mbali wakiwemo watoto yatima na wenye mazingira magumu leo Agosti 21, 2022.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Nuru Zanzibar, ambayepia ni Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib,akiwa katika picha ya pamoja na Watoto yatima kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Mkoani Pemba, katika ziara yake ya kuwasalimia, kuwafariji na kuwagawia misaada wananchi mbali mbali wakiwemo watoto yatima na wenye mazingira magumu, leo Agosti 21, 2022 mara baada ya kikao kilichofanyika Skuli ya Mwambe Mkoa wa Kusini Pemba. Kulia kwa Mama Zainab ni Bw. Khatib Juma Mjaja (Mkuu wa Wilaya ya Mkoani-Pemba) na Kushoto ni Bi Fatma Khamis Ali, (Sheha wa Shehia ya Mchakwe).
(Picha na Abeid Khamis - Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar)

MWENYEKITI wa Taasisi ya Nuru Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib, amesema ulinzi kwa watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji, ni wajibu wa kila mtu, ili kuwekeza katika ustawi bora wa jamii.


Mama Zainab ambaye ni Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo, kwa nyakati tofauti, katika Ziara yake ndani ya Wilaya ya Mkoani wakati wa kukamilisha Ziara yake Kisiwani Pemba, akiwasalimia, kuwafariji na kuwagawia misaada wananchi mbali mbali wakiwemo watoto yatima na wenye mazingira magumu.


Amesema kuwa wimbi la vitendo vya ukatilli Nchini ni adui wa moja kwa moja wa maisha ya watoto, na kwamba linadhoofisha kwa kiasi kikubwa maendeleo na ustawi bora wa jamii katika visiwa vya Unguja na Pemba.


Aidha amewashauri watoto kutokuwa 'wasiri' pindipo watakabiliwa na tishio lolote, na kwamba yawapasa kuwafichua wote ambao wanawafanyia vitendo vibaya ama kuashiria.


"Sambamba na haya tutambue kwamba ni wajibu wetu sote wazazi kuacha muhali wa kuwaficha wahalifu wa vitendo hivyo vya ukatili kwa kuhofia lawama za kifamilia au jamii", ameeleza Mama Zainab.


Aidha amewataka wazazi kutokuwatumia ama kuwaruhusu watoto kujihusisha na ajira za utotoni.


"Kipindi hichi cha uchumaji wa karafuu baadhi ya watoto wanaonekana katika zoezi hilo kwalengo la kujipatia pesa, ila msimu ukiisha wataanza kujikita katika vitendo vya uhalifu ili tu waendelee kupata pesa, hili ni kosa la wazazi na wanaowaajiri, na inabidi likemewe", amefafanua Mama Zainab


Akizungumzia suala la usajili wa watoto yatima unaoendelea sasa katika Taasisi ya NURU, Mama Zainab amesema kuwa jambo hilo ni muhimu na litasaidia kuwapatia huduma kwa ufanisi zaidi pamoja na kuwahamasisha wafadhili.


"Wanaojitolea kuwafadhili watoto yatima wanakuwa na dhamira njema hivyo kunahitajika utaratibu wa wazi ili kuwajengea imani zaidi ya kuwasaidia walengwa", amebainisha Mama Zainab.


Akitoa salamu zake kwa niaba ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Bw. Khatib Juma Mjaja amesema jamii yake ni miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya watoto yatima na wenye mahitaji maalum hivyo ujio wa Nuru Foundation chini ya Mwenyekiti wake Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais ni faraja na msaada mkubwa kwao.


Mjaja amesisitiza haja ya viongozi kuwa karibu na jamii ya wenye uhitaji hususan watoto yatima ili kuwajengea imani na furaha na kuwaepusha kujiingiza katika makundi ya kihalifu.


Katika ziara yake Mama Zainab, amekutana na watoto yatima na wenye mazingira magumu kutoka Wilaya ya Wete, Chake chake, Micheweni na kukamilisha Wilaya Mkoani kisiwani Pemba.

No comments: