Costech yazindua Karakana ya Mzee Pwagu

 MATUMAINI ya Watanzania kwa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ya kuendeleza, kukuza na kulea wabunifu, na watafiti kwenye teknolojia na sayanzi nchini Yazidi


Hayo yametanabaishwa mapema wiki hii wakati Costech ilipozindua Karakana iliyobuniwa na mzee John Fute maarufu kwa jina la Pwagu, karakana hiyo yenye jina la Pwagu Innovation Clinic ilibuniwa na Mzee Pwagu, Mkoani Njombe ambayo imeajiri vijana zaidi ya watano.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tume hiyo Emmanuel Girimwa Afisa Uratibu wa Utafiti wa Costech amesema Costech iliona ubunifu wa Pwagu utakuwa tija kwa wakazi wa Njombe na mikoa ya jirani na kuja kuwawezesha vijana kujiajiri kuendesha familia zao.

Amesema kuwa mbunifu huyo alisaidiwa na Tume hiyo kuanzisha karakana hiyo na kuwasaidia ujuzi yeye na wasaidizi wake.

“Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, tumekuja hapa kwa kazi moja kwa ajili ya kufanya uzinduzi wa Karakana ya Pwagu innovation clinic ambayo wazo lake liliibuliwa mwaka 2019 baada ya kupata taarifa kuhusu kazi zake nyingi zinazofanywa, tukaamua kuja kutembelea, tukashauriana na watu wa SIDO “amesema Girimwa.

Amesema kuwa hilo ni jukumu la msingi la Tume hiyo “Sisi kama Costech kazi yetu ni kuinua na kuendeleza ubunifu mbalimbali nchini tukaona fursa kubwa na tukasema tutamsaidia”

Ameainisha kuwa, Costech ilitoa kiasi cha Shilingi milioni 25 kwa ajili ya kununua mashne na gharama za mwanzo za uendeshaji.

Amesema kuwa baadaye Taasisi hiyo ilipeleka hela Sido kiasi hicho hicho cha shilingi milioni 25 na kumuunganisha na watu wa Sido ili aweze kuongeza zaidi ujuzi wake na karakana ifanye kazi.

"tumepeleka hela Sido sh. milioni 25 wamenunua mashine tatu. Mashine ya kuchonga vipuri na mashine ya kukata chuma. Leo tumekuja kukabidhi ili karakana ianze kufanya kazi.” amesema

Costech haijaishia hapo imempa mtaji wa awali wa kiasi cha shilingi milioni moja na nusu 1.5 kwa ajili kuanza kazi kwenye karakana hiyo.

“ Hela hiyo tuliyompatia ni kama kianzio kwa kununua vifaa na gharama zingine ndogo ndogo za uendeshaji ili kuhakikisha kuwa karakana inafanya kazi.”

Girimwa amesema kuwa Karakana hiyo itaweza kuwaajiri vijana wengi , na kwamba karakana hiyo itatengeneza mashine za kuvuna Parachichi na kukata majani kwenye mashamba.

Kwa upande wake, mzee Pwagu ameishukuru Costech kwa kumfadhili na kwamba kupitia karakana hiyo atawaajiri vijana wengi wa Njombe na kuwafundisha.

Amesema kuwa Karakana hiyo inakwenda kuimarisha kilimo cha Parachichi na chai ambapo ametengeneza mfumo wa maji kwa ajili ya umwagiliaji katika kilimo.

“Kutokana na mashine hizi ninaahidi nitatengeneza mashine nyjngi na baada ya mwaka mmoja mtaona mapinduzi makubwa sababu fursa ipo kwani sasa hivi hata kuvuna maparachichi juu watu wanashindwa wanavuna kwa kupiga miti, mimi nimebuni kikapu ambacho kina mkasi unapandisha na fimbo kinakata na kushusha kiusalama vila kuwepo uharibifu wa maparachichi" amesema.

Kelvin Kimaro, mmoja wa wanafunzi kwenye Karakana ya Mzee Pwagu amesema kuwa amejifunza kutengeneza Pump ya kufanya umwagiliaji kwenye mashamba

“Uwezeshaji wa vijana kwenye ubunifu ni jambo zuri kwa kuwa tunakuwa tumepata vitendea kazi na shughuli hizi zitatusadia kupata chakula cha kulea watoto na sisi kuendesha maisha yetu.”

Abel Ongoli mtoto wa mzee Pwagu,amesema kuwa amejifunza teknolojia kwa baba yake lakini jitihada za serikali zimewatia ari ya kuendeleza ubunifu hasa kwenye kilimo.

“Tunashukuru sana msaada mnaotupatia lakini bado tunahitaji msaada zaidi ili tuweze kuwa na vifaa vya kazi vingi kuongeza ujuzi kwani vifaa vikiwa vingi hivyo ujuzi utaongezeka kwani tunajifunza zaidi.” Amesema Ongoli
Kelvin Kimaro (mwanafunzi wa Mzee Pwagu) mwenye Tisheti ya mistari akionyesha namna mashine hiyo inavyochonga vipuri na kukata chuma.

No comments: