MILIONI 237 ZALIPWA KUPISHA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI MSHIKAMANO
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala amesema Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejizatiti katika kuboresha huduma za maji kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani na uwezo huo wanao.
Pia, DAWASA wameweza kulipa fidia kwa wananchi saba (7) waliokubali kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa tenki la Mshikamano kwa jumla ya Shilingi Milioni 232.6
Amesema, DAWASA imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kusikiliza changamoto za maji katika mkoa huu.
Makala amesema, DAWASA wanafanya kazi kubwa ikiwemo kufikisha huduma za maji kwa kujenga miradi mikubwa ya maji na kuboresha usambazaji wa maji katika maeneo yasiyokuwa na mtandao.
Akiwa katika hafla ya ulipaji wa fidia kwa wananchi wa Mshikamano, Makala amesema DAWASA inatekeleza kauli ya Rais Samia Suluhu ya kuzitaka mamlaka za maji kukamilisha miradi ya maji ndani ya miezi tisa (9).
Makala amesema, “Nilivyopigiwa simu na DAWASA kuna zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wa Mshikamano waliokubali kutoa maeneo yao ili kupishana mradi sikusita kukubali na kuja kushuhudia.”
Amesema, mradi wa Mshikamo ni mkubwa na unaenda kuondoa kero ya maji katika Jimbo la Kibamba na maeneo ya karibu ambapo unagharimu kiasi cha Bilion 5.4
“DAWASA wamefanya kazi kubwa sana, leo nimefika hapa Bohari Kuu nimeshangaa nimekuta imesheheni vifaa, wakati nikiwa Naibu Waziri wa Maji eneo hili halikua na vifaa kabisa,” amesema Makala.
“Naamini kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu Cyprian Luhemeja miradi mikubwa ya maji inaenda kutekelezwa na kumaliza changamoto ya maji kwa kutumia kauli ya Kumtua mama ndoo kichwani,”
Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Mradi wa mshikamano unaenda kutekelezwa baada ya wananchi kukubali kuachia maeneo yao ili kupisha ujenzi wa tenki la maji.
Amesema, tayari vifaa vya mradi huo vimeshaanza kuwasili katika bohari kuu iliyopo Boko tayari kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa majj wa Mshikamano Katika Jimbo la Kibamba.
“Mradi huu unaenda kutekelezwa na wananchi leo watakabidhiwa mfano wa hundi zao za malipo ya fidia baada yakupisha maeneo yao ili ujenzi uendelee,” amesema.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Kibamba Issa Mtemvu amesema DAWASA wanafanya kazi kubwa sana na kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa Mshikamaano unaenda kumaliza zile kelele za wananchi kuhusu upatikanaji wa maji ndani ya jimbo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe ameushukuru uongozi wa DAWASA kwa hatua kubwa wanazozifanya za kuwafikia wananchi wote ikiwemo wale wa pembezoni mwa mji.
DAWASA imeendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Hassan Suluhu kwa kuwafikia wananchi wote ambapo mradi wa Mshikamo utaondoa kero kwa wananchi wa Makabe, Mshikamano na Malambamawili.
No comments: