NIMR YAWAPIGA MSASA WATAFITI WACHANGA ILI KUKUZA UFANISI WAO KAZINI

 TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) inaendesha mafunzo ya siku 10 kwa Watafiti wake wachanga ili kukuza ufanisi wa kazi, ambapo suala la uandishi wa rasimu bora za tafiti za afya zinazozingatia maadili ya Taifa ya Utafiti nchini linapewa kipaumbele kupitia mafunzo hayo.


Akiwasalimu Washiriki wakati mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa Yunus Mgaya amesema Utafiti ni kazi ya kujituma inayohitaji ubunifu na uwajibikaji mkubwa, ndiyo maana NIMR imejiwekea mkakati wa kudumu wa kutoa mafunzo kwa watafiti wachanga wakiwemo waajiriwa wapya na watafiti waliohamia katika taasisi hiyo.

Profesa Mgaya amesema fedha za kutekeleza mkakati huo zinatokana na bajeti maalum za mafunzo zilizotengwa kupitia miradi mbalimbali ya utafiti inayotekelezwa nchini katika vituo vyote vya utafiti vya NIMR.

“Natumaini ndani ya hizi siku kumi, mtakamilisha rasimu za maandiko ya utafiti wa afya (Health Research Proposals) yenye hitajio la utafiti ili kujibu changamoto mlizoziibua awali katika afya ya jamii. Yachukulieni mafunzo haya kwa umuhimu mkubwa wa kipekee ili mtakapohitimisha mafunzo, mkaboreshe maandiko hayo na kuyaombea fedha za utafiti kwa wafadhili”. Profesa Mgaya alifafanua huku akiwswaasa Watafiti.

Mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa CEEMI-NIMR jijini Dar es Salaam yanashirikisha watafiti 27 kutoka katika Vituo saba vya utafiti vya NIMR vilivyopo mikoa ya Tanga, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Tabora na Dar es Salaam. Watafiti wawili kati yao wanatoka katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma (BMH) kama hatua ya NIMR ya kuboresha ushirikiano katika utafiti na wadau wake kutoka katika hospitali mbalimbali nchini.

Awali, Mratibu Mkuu wa Mafunzo ya Watafiti wachanga wa NIMR Bwana Jonathan Mcharo amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watafiti wachanga katika uandishi wa maandiko (Rasimu) ya tafiti za afya (Health Research Proposals) yenye viwango vinavyokubalika na yanayozingatia maadili ya nchi katika utafiti.

Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Mkurugenzi mratibu wa taarifa na mawasiliano ya kitafiti-NIMR Dakta Ndekya Oriyo na yanatarajiwa kufungwa tarehe 10 Septemba, 2021.

Mkurugenzi Mkuu NIMR Profesa Yunus Mgaya (aliyesimama) akiwasilimu Watafiti wachanga wa NIMR wanaoshiriki mafunzo ya kujenga uwezo wa uandishi wa maandiko ya Kitafiti, Maadili Bora na njia mbalimbali za kufanya Utafiti wa Afya nchini.
Baadhi wa Watafiti wanaoshiriki mafunzo hayo wakisikiliza neno kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa Yunus Mgaya.
Mratibu Mkuu wa Mafunzo kwa Watafiti wachanga wa NIMR Bwana Jonathan Mcharo akitoa maelezo mafupi kuhusu mafunzo hayo wakati Mkurugenzi Mkuu wa NIMR Profesa Yunus Mgaya alipowatembelea Watafiti hao kujionea maendeleo yao katika mafunzo hayo kwa vitendo. Mafunzo hayo ya siku 10 yalianza rasmi tarehe 30 Agosti 2021 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 10 Septemba 2021.
Mratibu Msaidizi wa Mafunzo ya Watafiti wachanga yanayoendelea jijini Dar es Salaam chini ya uratibu na NIMR na CDC; - Bi. Sia Malekia akifuatilia kazi katika vikundi vya uaandaji wa andiko la utafiti wa kisayansi wa afya kwa Watafiti wachanga wa NIMR wanaohudhuria mafunzo hayo.
Mkufunzi wa Mafunzo ambaye ni Mtafiti Mwandamizi kutoka NIMR Bwana Mathias Kamugisha (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kuhusu njia mbalimbali za kufanya tafiti za afya kwa Watafiti wachanga wa NIMR Muhimbili wakati wa mafunzo hayo yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Maabara ya Sayansi kutoka Kituo cha Utafiti cha NIMR Mabibo jijini Dar es Salaam Dakta Mwanaidi Kafuye, akipata maelezo kuhusu utekelezaji wa kazi ya kikundi ya kuandaa rasimu ya andiko la utafiti wa afya kwa watafiti wachanga wa NIMR wanaoendelea na mafunzo yaliyoandaliwa na NIMR kwa kushirikiana na CDC.
Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo kutoka hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, Bi Monica Kesi akijitambulisha kwa Washiriki wa Mafunzo hayo. Hospitali ya Benjamin Mkapa ni moja ya Wadau wakuu wanaoshirikiana na NIMR katika kazi mbalimbali zikiwemo za Utafiti wa Afya.

No comments: