DKT SERERA AZINDUA UGAWAJI VITAMBULISHO SIMANJIRO

Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Serera amezindua ugawaji wa vitambulisho vya Taifa, ambapo watu 37,835 wa eneo hilo watapatiwa vitambulisho hivyo vipya.

Dkt Serera amewataka wananchi wa Simanjiro ambao vitambulisho vyao vimekamilika kujitokeza kwa wingi kufutilia kwenye kata zao.

Amesema wananchi wanapaswa kuchukua vitambulisho vyao japokuwa walijiandikisha miaka mitatu au minne iliyopita na vitambulisho vyao kupatikana hivi sasa.

Amesema awali ofisa wa mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (Nida) wilaya ya Simanjiro Hamida Ullaya alikuwa peke yake ila hivi sasa ameshaongezeka mfanyakazi mwingine.

"Hivi sasa wafanyakazi wa Nida watakuwa wawili hivyo shughuli za upatikanaji wa vitambulisho zitafanyika kwa urahisi," amesema Dkt Serera.

Ofisa wa Nida Wilaya ya Simanjiro, Hamida Ullaya amesema watu 96,750 walijiandikisha kwenye eneo hilo ili wapatiwe vitambulisho hivyo.

Ullaya amesema hadi hivi sasa vitambulisho vilivyotolewa ni vya watu 58,935 waliojiandikisha kwenye eneo hilo.

Amesema vitambulisho hivyo vitapelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo walipojiandikisha ambapo wananchi hao wanapaswa kuvichukua.

Mkazi wa kata ya Orkesumet, John Mollel ameishukuru serikali kwa kuwapatia vitambulisho hivyo, ambavyo walivisubiri kwa muda mrefu baada ya kujiandikisha.

Mollel amesema kupitia vitambulisho hivyo, wanaweza kuvitumia kwa maendeleo mbalimbali ikiwemo kupata ithibati ya kutambulika.

No comments: