DARASA LA SABA KUANZA MITIHANI KESHO. NECTA WATOA ONYO KALI
WANAFUNZI 1,132,143 wa darasa la saba kutoka shule 17,585 za Tanzania bara, wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kesho Jumatano Septemba 8 na keshokutwa Alhamisi Septemba 9, 2021.
Kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 547,502 sawa na asilimia 48.36 na wasichana ni 584,641 sawa na asilimia 51.64.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 7, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kuanza kwa mitihani hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde amesema idadi ya masomo yatakayotainiwa imeongezeka na kufikia sitakutoka matano
" Katika Mtihani huu, idadi ya masomo imeongezeka kutoka masomo matano yaliyotahiniwa mwaka 2020 kuwa masomo sita. Somo lililoongezeka linaitwa Uraia na Maadili". amesema Dkt Msonde
Ameongeza maboresho hayo yamezingatia utekelezaji wa mtaala unaotumika kwa watahiniwa tangu walipoanza masomo yao na kuongeza kuwa masomo mawili pia yameboreshwa maudhui yake ambapo sasa somo la Sayansi litaitwa Sayansi na Teknolojia na somo la Maarifa ya jamii litaitwa Maarifa ya Jamii na Stadi za kazi.
Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia, hisabati maarifa ya jamii na stadi za kazi pamoja na Uraia na Maadili
“Kati ya watahiniwa 1,132,143 waliosajiliwa kufanya mitihani hiyo mwaka 2021, watahiniwa 1,079,943 sawa na asilimia 95.39 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 52,200 sawa na asilimia 4.61 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,” amesema Dkt Msonde
Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 23,327 ambapo kati yao 108 ni wasioona, 951 wenye uoni hafifu, 739 wenye ulemavu wa kusikia, 358 ni wenye ulemavu wa akili na 1,171 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili.
"Mwaka 2020 idadi ya watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 1,029,950 na hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 108,193 sawa na asilimia 10.57 kwa mwaka huu 2021 ukilinganisha na mwaka jana," amesema Dkt Msonde.
“Maandalizi kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalumu za ‘OMR’ za kujibia mtihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika halmashauri na manispaa zote nchini,” amesema Dkt Msonde.
Aidha ametoa wito kwa wasimamizi wateule kufanya kazi yao ya usimamizi kwa makini na uadilifu huku wakizingatia kanuni na miongozo waliyopewa huku wakihakikisha wanalinda haki ya watahiniwa wenye mahitaji maalumu
Katibu mtendaji huyo amewataka wamiliki wa shule wote kutambua shule zao ni vituo maalumu vya kufanyia mtihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi katika kipindi chote cha mitihani.
“Baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajidhilisha pasipo na shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya Taifa,” amesema Dk Msonde.
Pia baraza linawaasa walimu wakuu, waratibu elimu kata na wamiliki wa shule kutojihusisha katika kupanga na kutekeleza njama za udanganyifu.
"Baraza la mitihani halitasita kimchukulia hatua Mwalimu Mkuu, Mratibu wa Elimu Kata Mmiliki wa shule, Msimamizi Mkuu au Msimamizi wa mkondo endapo itabainika wamehusika kusababisha udanganyifu kutokea shule yoyote," amesema Dkt Msonde.
No comments: