SERIKALI YATENGA SH BILIONI 570 KWA AJILI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU KWA MWAKA MPYA WA MASOMO
Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imetenga kiasi cha Sh Bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu nchini ikiwa ni ongezeko la takribani Sh Bilioni 106 kulinganisha na kiasi cha Sh Bilioni 464 ambacho kilitolewa kwa mwaka wa masomo uliopita.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe alipokua akizungumza na wandishi wa habari katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa ambapo wanahabari walifika kujionea maboresho na ukarabati uliofanywa na Serikali chuoni hapo.
Prof Mdoe amesema ongezeko hilo la fedha za mkopo wa wanafunzi wa elimu ya juu ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu ambapo lengo lake ni kuona kila mwanafunzi mwenye sifa ananufaika.
" Kwenye sekta ya elimu ni wazi tumepiga hatua kubwa sana, mwaka 2015 kiasi ambacho kilitengwa kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ni Sh Bilioni 348, mwaka 2020/21 kiasi cha Sh Bilioni 464 kilitolewa kwa wanufaika wa mkopo na sasa katika Bajeti hii mpya ya awamu ya sita kwenye mwaka wa masomo unaoanza Oktoba mwaka huu tumetenga Sh Bilioni 570 ikiwa ni ongezeko la Sh Bilioni 106 kulinganisha na mwaka jana," Amesema Prof Mdoe.
MAFANIKIO YA UJENZI NA MIUNDOMBINU
Akizungumzia mafanikio ya ujenzi na miundombinu kwenye Vyuo Vikuu nchini, Prof Mdoe amesema jinsi udahili wa wanafunzi unavyoongezeka ndivyo mahitaji ya miundombinu na vifaa vya tafiti na ufundishaji unavyoongezeka.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imefanya jitihada za kufanya maboresho ya miundombinu hiyo ikiwemo Mabweni, Madarasa, Maabara na Kumbi za mihadhara kwenye vyuo mbalimbali nchini.
Mathalani katika Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA) Serikali imefanya ujenzi mkubwa wa jengo la maabara ambalo ndani yake kuna maabara nane tofauti huku likiwa na uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 3200 kwa wakati mmoja lakini pia kukiwa na Ofisi tofauti tofauti zenye uwezo wa kubeba wafanyakazi 38.
" Maboresho yamefanyika makubwa katika vyuo vyetu, tukizungumzia Chuo cha Mzumbe tumejenga Mabweni yenye kubeba wanafunzi 1,000 na ukumbi wa mhadhara wenye kuchukua wanafunzi 300 kwa wakati mmoja.
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam napo wote ni mashahidi wa ukarabati mkubwa uliofanyika kuanzia ujenzi wa Hosteli maarufu za Magufuli, ukarabati kwenye Bweni namba mbili, nne na tano pia tumejenga maabara kubwa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja," Ameeleza Prof Mdoe.
MUELEKEO WA 2021 HADI 2025
Akizungumzia uelekeo wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia katika eneo la Elimu ya Juu nchini, Prof Mdoe amesema serikali inatarajia kupokea kiasi cha Sh Bilioni 985 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi.
Amesema Agosti 16 Waziri wa Fedha atasaini makubaliano na Benki ya Dunia kwa ajili ya ufadhili wa fedha za mradi huo ambao utatekelezwa kwenye Vyuo Vikuu vyote vya umma nchini na vyuo vishiriki.
Prof Mdoe amesema mradio huo wa miaka mitano pia utatekelezwa kwenye Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Bodi ya Mikopo (HELSB) na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
"Tunatarajia kupata kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 425 sawa na Sh Bilioni 985 kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi, lengo letu ni kuweza kuzalisha wanafunzi wenye taaluma stahiki kulingana na Soko la Dunia pamoja na kusomesha wahadhiri nje ya Nchi lakini pia kutoa mafunzo kazini ili kuwawezesha wataalamu wetu kuendana na mabadiliko ya teknolojia," Amesema Prof Mdoe.
Ameongeza kuwa asilimia 70 hadi 80 ya fedha hizo itatumika kwenye ujenzi mkubwa wa vyuo sambamba na kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye vyuo hivyo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe (mwenye tai Nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa mkoani Iringa na wandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akizungumza na watendaji wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa mkoani Iringa na Wandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali nchini. Kulia ni Naibu Rasi wa Mkwawa, Dk Fikira Kimbokota.
No comments: