KATAMBI AWASHUKIA VIONGOZI CHADEMA
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana na Ajira) Mhe.Patrobas Katambi, amewashukia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanaodai Katiba mpya, akisema madai hayo ni uchu wa vyeo na hayalengi maslahi ya taifa.
Amesema anashangazwa kuona wanaodai katiba mpya sasa ndiyo waliosusia vikao vya bunge la Katiba wakati wa serikali ya awamu ya nne na kuongeza kuwa, walifanya hivyo baada ya kuona ya kwao hayajafanikiwa.
Katambi aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, wakati wa mkutano wake na wandishi wa habari, uliolenga kutoa ujumbe wa serikali kwa vijana nchini.
Alisema madai hayo ya katiba mpya yanalenga watu fulani kufanikisha kuingiza mambo yao ndani yake ili yawasaidie kupata vyeo na kushinda uchaguzi wala si maslahi ya taifa.
“Wanaodai katiba mpya leo ndiyo hao waliokimbia vikao vya bunge la katiba wakati wa serikali ya awamu ya nne, kwa sababu walitaka yao yaingie waliposhindwa wakaamua kuvuruga mchakato,” alisema.
Katambi ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alifafanua kuwa mchakato wa katiba mpya wa awali uliigharimu serikali zaidi ya sh. bilioni 200 bila mafanikio.
Alieleza kwa sababu watu fulani walitaka ndani ya katiba hiyo, kuhusishwe mambo yao badala ya maslahi ya taifa, iliposhindikana walikimbia bunge na kubadili mtazamo.
“Wakati huo sisi tulikuwa wanasheria na wanaharakati wa mambo hayo, baada ya kukimbia bunge la katiba wanayoidai sasa wakaamua kujiunga na kutengeneza UKAWA ambao ulihusisha muunganiko wa vyama kadhaa vya upinzani,” alisema.
Alifafanua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, muungano huo walikubaliana kutoa mgombea mmoja wa urais na wakati wakivutana, kuna chama kilikuwa na mgombea wake mfukoni na hivyo baadaye alipendekezwa.
Alibainisha kuwa kabla ya uchaguzi na baada ya kumpendekeza mgombea wa urais ndani ya UKAWA kulikuwa na mvutano mkali wa kuunda Baraza la Mawaziri, ambapo kila chama kilitaka Waziri atoke ndani yake.
“Angalia mgogoro wa kugombea vyeo ulianza kabla ya ushindi, vyama viligombana nani awe Waziri Mkuu kila chama kikihitaji atoke kwake, viligombea wizara mbalimbali na baada ya mvutano mkali Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR Mageuzi vilijitoa na vingine kufuata”.
Aliongeza, “Sasa fikiria hawa waliogombea maslahi na vyeo ndiyo leo wanadai katiba mpya unadhani wanalenga maslahi ya nani, wanachohitaji ni kwamba Katiba iguse mambo yao sio masuala ya kitaifa”.
Alieleza kuwa hitaji la katiba mpya kwa wengi linahusu tume ya taifa ya uchaguzi, ili washinde nafasi za uongozi na wapate vyeo na kwamba huo ni mwenendo wao wa siku zote.
“Wakishindwa uchaguzi wanadai katiba mbaya, ila wakishinda wanakaa kimya, hata Mahakamani akishitakiwa mtu mwingine ni mkosaji wakishtakiwa wao wanadai wameonewa, mara katiba mbaya, mara wananyanyaswa,” alisema.
Alifafanua kuwa anatambua kwamba madai ya katiba mpya yameanza sasa kwa kuwa wanataka kuwalaghai watanzania kuwa ndiyo wanaodai ilhali ni hitaji lao.
Aidha, aliwataka vijana na Watanzania wote kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa nchi na masuala ya kisiasa waanze kuyafanya mwaka 2025.
Mbali na hayo, Naibu Waziri huyo, alieleza kuhusu utekelezaji wa uanzishwaji wa baraza la vijana ambapo tayari michakato imeanza yakiwemo mabadiliko ya sera ya vijana ya mwaka 2013.
Kuhusu chanjo ya covid-19, aliwasisitiza vijana kuacha kuchanganya sayansi na siasa na badala yake watumie tafiti za kitaalamu kujiridhisha na anayepinga aje na hoja za kitafiti.
Hata hivyo, alisema katika kupambana na dawa za kulevya hadi sasa serikali ina vituo 11 vyenye waathirika 10,560 wanaolelewa huku hatua za udhibiti wa vipenyo vya dawa hizo zikiimarishwa.
Pamoja na hayo, alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha kijana akikosa ajira anapata kazi, kwani kazi zipo nyingi isipokuwa baadhi yao huchagua.
Aliongeza kuwa katika ajira kwa vijana, nyingi ziKmezalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
Akitaja hatua zilizochukuliwa na serikali kusaidia vijana, alisema utoaji wa mikopo inayotokana na mapato ghafi ya halmashauri ambapo hadi sasa zaidi ya sh. bilioni 30 zimetengwa.
Alisema mambo mengine ni ujenzi wa shule, utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kugharimia mafunzo ya elimu ya ufundi kwa vijana na kuwajengea uzoefu wa kazi wahitimu wa vyuo.Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana na Ajira) Mhe.Patrobas Katambi akizungumza masuala ya vijana na mwelekeo wa Serikali katika kushughulikia masuala yanayohusu vijana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Agosti 14, 2021 katika Ofisi za PSSSF Jijini Dar es Salaam.kulia Mkurugenzi wa Uhamasishaji wa Habari Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Bw.Jumanne Isango (Picha Zote na Emmanuel Massaka wa Michuzi TV)
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda (kulia) akizungumza kuhusu masuala ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi wakati wa mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam.kushoto Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana na Ajira) Mhe.Patrobas Katambi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana na Ajira) Mhe.Patrobas Katambi (katika)akifafanua jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo Agosti 14, 2021 katika Ofisi za PSSSF Jijini Dar es Salaam.(Picha Zote na Emmanuel Massaka wa Michuzi TV)
No comments: