CRB yakopesha makandarasi hadi milioni 100
Naibu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), David Jere akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo mkoani Morogoro. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya CRB Consolata Ngimbwa na Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo Joseph Tango.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Consolata Ngimbwa katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya siku tatu kwamakandarasi wazalendo yanayoendelea mkoani Morogoro.
Mratibu wa Mafunzo wa Bodi ya Makandarasi (CRB), Neema Fuime kushoto akiwa na washiriki wengine kwenye mafunzo hayo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo yanayoendelea mkoani Morogoro.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MFUKO wa kuendeleza makandarasi wazalendo Contractors Assistance Fund (CAF), umeendelea kuimarika na sasa unauwezo wa kukopesha makandarasi hao hadi shilingi milioni 100.
Hayo yamesemwa leo mkoani Morogoro na Naibu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi David Jere, kwenye mkutano wa mafunzo wa siku tatu kwa makandarasi.
Alisema CRB ilianzisha mfuko huo miaka ya hivi karibuni kwaajili ya kuwakopesha makandarasi kwaajili ya kuanza kazi mara moja wanapopata miradi na walianza na shilingi milioni 50 tu.
“Kwa sasa mfuko wa makandarasi umeendelea kuimarika na una uwezo wa kuwakopesha kila mmoja hadi sh milioni 100 kutoka shilingi milioni 50 za awali hivyo hii ni fursa kwenu ukiwa na sifa unakopeshwa unaanza kazi,” alisema
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Consolata Ngimbwa aliwataka makandarasi kuungana na kuanzisha chama kimoja chenye nguvu ambacho kitakuwa sauti yao wanapokuwa na shida za kuwasilisha serikalini.
Alisema watu wa tasnia mbalimbali kama wahandisi, wasanifu majengo, wakadiriaji majenzi na hata waendesha boda boda wanavyama vyao ambavyo vina nguvu.
“Kila siku tunazungumzia suala hili hili sijui tumekwama wapi sasa naomba ifike wakati tuseme inatosha, muwe na chama chenu chenye nguvu tusiwe tunazungumza jambo hili hili kila tukikutana,” alisema
“Wakati serikali ilipoamua kutumia force account tuliyumba sana na nilidhani tumejifunza kwa yaliyotokea wakati huo kwamba ungekuwa wakati mwafaka wa kukutana na kujadiliana namna ya kuwa na sauti moja lakini naaona bado,” alisema.
Pia aliwataka makandarasi hao kuacha kuomba zabuni kwa bei ya chini ili kuwavutia watoaji wa zabuni kwani uzoefu unaonyesha wanapozipata wamekuwa wakishindwa kuzikamilisha na wengine kukimbia.
Alisema baadhi ya makandarasi wamekuwa wakijaza hela ndogo kama mbinu ya kushinda zabuni lakini wanapopata kazi hizo wanashindwa kuzikamilisha kwa wakati na wengine kushindwa kuzikamilisha kabisa.
“Jazeni zabuni vizuri tena kwa uhalisia msijaze tu ilimpate zabuni lakini mwishowe zinawashinda, hapa katikati tuliyumba sana baada ya serikali kuanza kufanyakazi zake kwa kutumia utaratibu wa force account sasa tumeanza kupata kazi za serikali tusifanye makosa, tuzifanye kwa weledi mkubwa,” alisema Ngimbwa.
Alisema CRB iliamua kuanza kutoa mafunzo hayo kwa makandarasi baada ya lawama nyingi kwamba makandarasi hao wamekuwa wakiweka bei ambazo hazina uhalisia.
Mhandisi Ngimbwa aliwasisitiza pia kufanyakazi kwa ubia na makandarasi wenzao na wanaposhindwa kujua namna ya kuzifanya wafike ofisi za bodi hiyo au kwa wataalamu kwaajili ya kuelekezwa namna ya kufanyakazi za aina hiyo.
“Wengi tunaingia kwenye kazi za ubia lakini tunashindwa sijui kwasababu hatuzijui au, uzuri wa kazi hizi ni kwamba mnaunganisha nguvu na kufikia vigezo vinavyohitajika na kama mkishindwa njooni CRB mtaelekezwa,” alisema
Mratibu wa Mafunzo wa CRB, ambaye ni Msanifu Majengo, Neema Fuime alisema mafunzo hayo ya mara kwa mara yanalenga kuwapa makandarasi wa ndani uwezo wa kujaza zabuni kitaalamu wanapoomba kazi.
Alisema awali baadhi ya watoa kazi walikuwa wakilalamika kuwa makandarasi wengi hawana uwezo wa kujaza zabuni ndiyo sababu CRB ikachukua jukumu la kuwapa mafunzo hayo.
No comments: