SERIKALI YATANGAZA KUWAITA KAZINI WATUMISHI 473 WA KADA YA AFYA NCHINI
Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imewataka watumishi 473 walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali katika kada ya afya nchini kuripoti katika Ofisi za Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto zilizopo Mirembe jijini Dodoma.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Prof Abel Makubi wakati akizungumza na wandishi wa habari ambapo amewataka watumishi hao kuripoti leo Julai 5 na mwisho wa kuripoti utakua Julai 9 mwaka huu.
Prof Makubi amesema wito huo wa Serikali kwa watumishi hao ni wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na watumishi wengine kufariki,kuacha kazi na waliokoma utumishi wao kwa kustaafu.
Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia Wizara hiyo kutoa kibali cha ajira za kada mbalimbali za Afya Kupitia tovuti ya Wizara mnamo Mei 12 Mwaka huu zilizotokana na watumishi kukoma utumishi Kutokana na sababu mbalimbali.
Prof Makubi amesema uteuzi wa watumishi hao umezingatia sifa na vigezo mbalimbali vilivyowekwa katika kuwapata watumishi hao.
" Kutokana na nafasi hizo 473 ambazo tulizitangaza tulipokea jumla ya maombi 19757 ambapo kati ya hayo maombi 4760 yalikosa sifa kutokana na kutokamilisha taratibu za uombaji ajira.
Wengi hawakukamilisha taratibu za uombaji kwa kushindwa kuambatanisha vyeti vya taaluma huku baadhi wakiomba nafasi ambayo sio taaluma yao hivyo maombi yao kutokidhi vigezo,hivyo basi maombi 9338 ndiyo yamekidhi vigezo na sifa za kuajiriwa na kati yao 473 ndio wakachagulia," Amesema Prof Makubi.
Prof Makubi ameeleza vigezo vilivyotumika kuwapata waombaji hao kuwa ni pamoja na kuzingatia waombaji wenye ulemavu,wenye ajira za mikataba ya muda, waombaji wenye umri chini ya miaka 45 na waombaji waliohitimu elimu ya mwaka 2018 na kurudi nyuma.
Kwa umuhimu huo amefafanua pia mgawanyo wa nafasi hizo 473 kwa kada mbalimbali kulingana na walivyopokea kutoka Ofisi-Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora kwamba katika kada ya Daktari bingwa idadi ya nafasi zilizohitaji kibali ni Saba na waliochaguliwa ni Saba.
"Daktari daraja la pili 23,Daktari wa meno 5,Afisa Muuguzi 17,Afisa Muuguzi msaidizi 67,nafasi ya Muuguzi 140,Afisa afya mazingira 3 na Afisa afya mazingira msaidizi 3.
Nafasi nyingine ni za Fundi sanifu vifaa tiba nafasi 1 , Fiziotherapia nafasi 2,Katibu wa afya 1,Famasia 7,Mteknolojia-Meno 3,Mteknolojia-Mionzi 5,Mteknolojia Maabala 10 ,Myeknolojia-Macho 5, Mteknolojia Msaidizi Maabala 8 Pamoja na Msaidizi wa afya 166," Amesema Prof Makubi.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Prof Abel Makubi akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo wakati akitangaza kuwaita kazini watumishi 473 wa kada mbalimbali za Afya.
No comments: