WMA yataka wananchi wahakiki mitungi ya gesi
WAKALA wa Vipimo (WMA), umewataka wananchi kuhakikisha wana hakiki mitungi ya gesi kama inaujazo sahihi ulioandikwa kabla ya kuondoka nayo wanapoinunua kwani kuna baadhi wauzaji hupunguza ujazo.
Meneja wa WMA Mkoa wa Kagera, Harrieti Lukindo, ameyasema hao leo, Juni 30 2021 alipokuwa akizungum kwenye maonyesho ya 45 yanayoendelea katika viwanja vya maonyesho ya kimataifa vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (sabasaba).
Amesema watanzania wengi wamekuwa hawana muamko wa kupima na kuhakiki ujazo wa mitungi yao ya gesi pindi wanaponunua, na hivyo kupelekea wao kupunjwa kwa kupata ujazo kidogo.
“Kwanza watanzania wengi hawaendi wenyewe wanawatuma watu wa boda boda ndiyo maana wanachukua bila kuipima, lakini unapaswa kuuhakiki mtungi wako kwenye mzani ambao kila muuzaji wa gesi anatakiwa kuwa nao kwa mujibu wa sheria,” amesema
Aidha Lukindo amesema WMA imekuwa ikifanya ukaguzi wa kushtukiza na mara kadhaa wamekuwa wakikuta baadhi ya mitungi ikiwa na upungufu wa ujazo uliaondikwa kwenye mtungi husika hivyo kumpunja mlaji.
“Lazima mnunuzi ajiridhishe kwamba mtungi wake haujachezewa ahakikishe alama ya kufungia (seal) kwenye mtungi husika haijafunguliwa kwasababu baadhi huwa wanapunguza kilo na kuhamishia kwingine,” amesema.
Kwa upande wake, Afisa Vipimo wa WMA, Mkoa wa Ilala, Glory Mtana amewataka watanzania wenye wasiwasi na mita zao za maji kutoa taarifa kwa mamlaka hiyo ili ziweze kuhakikiwa kama zina ubora unaokubalika kisheria.
Alisema miongoni mwa mambo wanayofanya kwenye maonyesho hayo ni kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakiki mita za maji ili wapate bili sahihi kutoka kwa mamlaka.
Amesema WMA imekuwa ikihakiki mita za maji ili kuhakikisha watanzania wanalipia kiasi sahihi wanachotumia na mamlaka husika kupata malipo yanayostahili, na kwamba ili kujua kwamba hii mita imehakikiwa lazima iwe na alama ya kufungia (seal) ya serikali na watu wanaofungiwa mita za maji wazingatie hilo ili wapate huduma sahihi.
Ameongeza kuwa, mbali na mita za maji, WMA pia imeishaanza kuhakiki mita za umeme ili kuhakikisha watumiaji wa nishati hiyo wanalipia kiasi tu walichotumia na si vinginevyo.
"Mita hizo za maji na umeme zimekuwa zikihakikiwa kwenye kituo cha Misugusugu Mkoa wa Pwani kabla ya kwenda kwa watumiaji ili kuepusha malalamiko kwa wananchi kuletewa bili isiyo sahihi huku pia wakihakiki mizani inayopima madini , kuhakiki vipimo katika sekta ya kilimo na kuhakiki bidhaa zilizofungashwa", amesema.
Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa Kagera Harriet Lukindo, akiwaelezea wananchi waliofika kwenye banda hilo kuhusu uhakiki wa mitungi ya gesi kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam.
No comments: