WATANZANIA WASHAURIWA KUWASAIDIA WALIOPATA TIBA YA SARATANI ILI KUOKOA MAISHA YAO,KUWAWEZESHA KUFIKIA MALENGO
Na Mwandishi Wetu
JAMII ya Watanzania kwa ujumla wameshauriwa kuwasaidia watu waliopata tiba ya saratani ili kuokoa maisha yao, kuwawezesha kufikia malengo yao na kuwa na furaha.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Tiba kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Mark Mseti katika maadhimisho ya kitaifa ya Shujaa wa Saratani, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini Jumapili, kwenye viwanja vya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Katika sherehe hizo zilizoandaliwa na asasi ya Shujaa Cancer Foundation inayotoa huduma kwa mashujaa wa saratani ya matiti, shingo ya kizazi na tezi dume, Dk. Mseti akisema: “Si kazi ndogo kuishi na saratani,tuokoe maisha ya mama aliyeachwa kwa sababu ya kuugua saratani, tuokoe maisha ya aliyekimbiwa na mchumba hata baba alitengwa kwa sababu tu ya kuugua saratani, saratani siyo kifo.”
Alisema ugonjwa wa saratani ni vita na kwamba mapambano ya ugonjwa huo yana historia ndefu nchini hivyo kila mtanzania ana wajibu wa kuisaidia jamii ya watu waliopatwa na saratani.
Akizungumzia ugonjwa wa saratani, Dk Mseti alisema una sababu kuu tano alizozitaja kuwa ni mionzi, kiurithi katika familia,kemikali, mtindo wa maisha pamoja na maambukizi mbalimbali.
Naye mkurugenzi mtendaji wa asasi ya Shujaa Cancer Foundation, Gloria Kida aliiomba serikali kushirikiana na asasi yake ili kuwawezesha mashujaa wa saratani kuishi maisha bora.
“Hii ni siku ya kutiana moyo, saratani isikatishe ndoto za maisha yetu, tukiiwahi tukatumia dawa inapona. Serikali iungane nasi mashujaa wa saratani, itusaidie kwani ushirikiano ukiwa mzuri maisha ya tunaoishi na ugonjwa huo yatakluwa mazuri na marefu,” alisema Gloria huku akiwashukuru madaktari, wauguzi na wahudumu wa afya kwa upendo na kujitoa kwao kuhudu,ia wagonjwa wa saratani.
Kuhusu asasi yake, Gloria alisema inalenga kuainisha changamoto zinazowakabili mashujaa wa sarstani kuwawezesha kuondoa changamoto zinazowakabili na kufikia malengo yao.
Katika tukio hilo, mashujaa wa saratani walitoa ushuhuda wa jinsi walivyogundulika kuugua, kunyanyapaliwa, kutibiwa hadi kupona ambapo sasa wanatamani kutimiza ndoto zao za maisha, baada ya kufutika kutokana na kuugua, wakiiomba serikali kuwapatia vitambulisho maalum vitakavyowawezesha kupata matibabu kwenye hospitali yoyote bure.
“ Miaka mitatu ioliyopita tulimuomba Waziri wa afya wakati huo (Ummy Mwalimu) tupatiwe vitambulisho tuweze kutibiwa bure popote nchini, hadi leo kimya. Tunaomba tena serikali ifikirie kufanya hivyo na sisi tuliotibiwa na kupona saratani, tunatkiwa kuwatia moyo wengine wanaougua kuwa kuna kupona. Saratani inapona.Tupewe nafasi ya kueneza ufanisi wa sayansi na zinapopatikana huduma,” alisema Faustine Luambano (65) aliyepona saratani ya tumbo.
No comments: