WASANII KUANZA KULIPWA MIRAHABA DESEMBA, 2021




Na Shamimu Nyaki, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuanzia mwezi Desemba mwaka huu wasanii wataanza kulipwa Mirabaha yao kupitia kazi za Sanaa zinazochezwa katika redio, runinga na mitandao ya kijamii.

Mhe. Samia amesema hayo Juni 15, 2021 Jijini Mwanza alipokuwa anazungumza na vijana wa Mkoa huo kwa niaba ya vijana wote nchini, ambapo amesema Sekta ya Sanaa, Utamaduni na Michezo inaajiri vijana wengi hivyo Serikali inendelea kuimarisha sekta hizo.

“Tumeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kusaidia timu zetu za Taifa, tumefuta kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika nyasi bandia, hivyo majiji manispaa changamkieni fursa hii kupata viwanja bora” amesisitiza Mhe. Samia.

Aidha, Mhe. Rais ametoa wito kwa Chama cha Mapinduzi kutumia fursa hiyo kuboresha viwanja ambavyo inavimiliki katika mikoa na majiji yote nchini ili kuweka mazingira sahihi ya kuendesha michezo nchini.

Vilevile ameiagiza Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo kuanzisha vituo vya michezo (Sports Academy) kila Mkoa ili kukuza vipaji na sekta ya michezo hapa nchini.

Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa wafanyabiashara na watoa huduma kutumia wasanii katika kutangaza huduma na biashara zao kwa kuwa wasanii wana wafuasi na ushawishi mkubwa katika jamii, huku akisisitiza vijana ambao wanavipaji kuvionyesha ili viwapatie ajira.

Kuhusu suala la kuwepo na Sports and Arts Arena Mhe Bashungwa amesema kuwa katika mwaka ujao wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kupata mtaalam mshauri ili kufanya upembuzi yakinifu ambao utaisaidia Serikali kutekeleza ujenzi huo.

Hata hivyo Mhe. Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuboresha Sekta ya Sanaa ambapo mpaka sasa taasisi za BASATA, Bodi ya Filamu na COSOTA zinafanya kazi eneo moja na mpango uliopo ni kuziunganisha taasisi za BASATA na Bodi ya Filamu ili kurahisisha utoaji wa huduma katika taasisi hizo kwa wadau wake.

No comments: