Waliochaguliwa JKT Mujibu wa Sheria Watakiwa Kuripoti Makambini
Na Mwandishi wetu- Dodoma
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Rajabu Mabele amewataka vijana wote waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria kwa mwaka 2021 ambao hawajaripoti na wale waliochanguliwa kwa awamu ya pili kuhakikisha wanaripoti kwa wakati katika makambi waliyopangiwa kufikia June 17, 2021 ili waweze kuanza mafunzo hayo kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Kanali Hassan Mabena leo Juni 10, 2021, Jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya JKT Chamwino mkoani Dodoma.
“Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria mwaka 2021 yataendeshwa kwa muda wa miezi mitatu tu, vijana hao walioitwa kupitia orodha ya pili na baadhi ya wale wa awamu ya kwanza ambao hawajaripoti hadi sasa wanatakiwa kuripoti makambi ya JKT waliyopangiwa mara moja”, alisisitiza Kanali Mabena
Akifafanua, Kanali Mabena amesema kuwa kwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (Physical disabilities) wanatakiwa kuripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuwahudumia.
Orodha kamili ya nyongeza ya majina ya vijana walioitwa , Makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo yaliyopo pamoja na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz.
Aidha, Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote walioitwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa.
Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Hassan Mabena akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo June 10, 2021 Jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya JKT kuhusu nyongeza ya vijana wanaojiunga na mafunzo ya JKT mujibu wa sheria ambao wamehitimu kidato cha sita mwaka 2021 ili waweze kuungana na vijana wenzao walioitwa hapo awali kuhudhuria mafunzo haya kwa mujibu wa sheria.(Picha zote na MAELEZO)
No comments: