WACHIMBAJI TANZANITE WAMUOMBA MAKONGORO AWASAIDIE WACHIMBE KITALU C

Pica ya pamoja.

Na Gift Thadey, Mirerani

WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani, wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere kufikisha kilio chao kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili wapatiwe eneo la kitalu C wachimbe wenyewe.

Wachimbaji hao walieleza hayo wakati Makongoro akikabidhi tuzo 19 za aina tatu kwa wachimbaji tisa, zilizotolewa na chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (Marema) Tawi la Mirerani.

Mwenyekiti mstaafu wa Marema, Sadiki Mneney amesema wachimbaji wadogo wana uwezo mkubwa wa kuchimba Tanzanite hivyo serikali iwapatie kitalu C na siyo wawekezaji wageni.

"Kitalu hicho kinamilikiwa na serikali tupewe wachimbaji wadogo, uwezo tunao badala ya wawekezaji kwani hata nchi zilizoendelea hawagawi kwa wageni wanachimba wenyewe." Amesema Mneney.

Amesema awali, eneo hilo la kitalu C lilikuwa linachimbwa na wawekezaji ila hivi sasa ifike wakati wachimbaji wadogo wapatiwe fursa ya kuchimba na kunyanyua uchumi wa watu wengi.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, amesema alifika kutoa tuzo za wachimbaji na kukaribishwa rasmi hivyo atarejea upya kwa ajili ya kikao kazi.

Makongoro amesema atakutana na wachimbaji hao ili wajadili kwa undani kwa pamoja suala la wachimbaji wadogo kupatiwa eneo la kitalu C ili wachimbe madini.

"Leo nimekuja tuu kukabidhi tuzo na kufahamiana ila nitapanga ziara rasmi ya siku tano kutembelea Wilaya ya Simanjiro hivyo tutakaa tuzungumze juu ya mambo ya madini." Amesema Makongoro.

Katibu wa Marema Tawi la Mirerani Rachel, Njau amesema wametumia fursa hiyo kuwaaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula, aliyestaafu na aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Zuwena Omary Jiri aliyeteuliwa kuwa RAS Shinyanga na pia wachimbaji tisa wamepatiwa tuzo 19 zilizopo katika vipengele viatu.

Njau amesema tuzo ya kwanza kwa wachimbaji hao ni ulipaji kodi kwa serikali na tuzo ya pili ni kujitolea michango Serikalini na kusaidia jamii inayowazunguka kwa ujumla.

Amesema tuzo ya tatu ni kwa wamiliki wanaoheshimu na kutekeleza mikataba ya wabia wao kwa kuwapatia asilimia ya mgao wao, kuwapatia vitambulisho na haki zao stahiki.

Amewataja wachimbaji hao ni Bilionea Saniniu Laizer, Mkurugenzi wa Chusa Mining Ltd, Joseph Mwakipesile, Mkurugenzi wa Gems and Rock, Joel Saitoti, Mkurugenzi wa California Camp, Deo Minja na God Mwanga Gems Co. Ltd.

Amewataja wachimbaji wengine ni mkurugenzi wa Iraqw Mining Ltd, Emmanuel Wado, Mkurugenzi wa Franone Ltd, Onesmo Mbise  na Eliaman Mgala.

No comments: