VIROBA VITATU VIKIWA NA DAWA ZA KULEVYA VYAKAMATWA DAR BAADA YA KUTELEKEZWA KWENYE 'PRADO'.

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanikiwa kukamata kilo 88.27 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine zikiwa ndani ya gari aina ya Toyota Prado iliyokuwa imetelekezwa barabarani.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam , Kamishina Jenerali wa Mamlaka hiyo Gerald Kusaya amesema dawa hizo zimekamatwa Juni 2 mwaka huu , saa saba usiku katika eneo la Kimara Korogwe na kukamatwa kwa dawa hizo kumetokana na ushirikiano wa mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Ameongeza dawa hizo zimekamatwa baada maofisa wa TRA kulitia shaka gari hilo na kuanza kulifuatilia ."Dereva wa gari hilo baada ya kugundua anafuatiliwa alitelekeza gari na kukimbia.Baada ya upekuzi wa kisheria kufanyika ndani ya gari kulipatikana na mifuko mikubwa mitatu aina ya sandarusi (viroba).

"Ndani yake ikiwa na pakti 12 za dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 12.25 pamoja na kontena za plastiki 73 ndani yake kukiwa na dawa aina ya Methaphetamine zenye uzito wa kilo 76.02,"amesema Kamishina Jenerali Kusaya.

Ameongeza upelelezi bado unaendelea ikiwemo kugundua mwenye gari hilo na mtandao wake na kwamba Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama iko macho, haijalala na kwamba wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya waache kwani , hawatabaki salama.

"Ama zao, ama zetu lakini watambue Mamlaka tuko kazi muda wote na lengo letu ni kukomesha kabisa biashara hi haramu.Tunaomba wananchi waendelee kutoa taariffa ili kwa pamoja tushirikiane kukomesha dawa hizo,"amesema.

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu kukamatwa kwa dawa za kulevya kilo 88.27 ambazo zilikuwa ndani ya gari ya aina ya Toyota Prado ambayo ilitekelezwa barabarani.

No comments: