MFUMUKO WA BEI WABAKI TULIVU, PATO LA TAIFA LATEGEMEWA KUKUA - DK.MWIGULU

MFUMUKO wa bei nchini umeendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo umepungua kutoka wastani wa asilimia 3.4 mwaka 2019 hadi asilimia 3.3 mwaka 2020.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwakilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 na mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2021/2022 Bungeni jijini Dodoma.

Ambapo amesema kuwa, mfumuko wa bei kubaki katika asilimia 3.3 mwezi Mei 2021 na kuendelea kuwa tulivu ni kutokana na upatikanaji wa chakula cha kutosha, kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani naa sarafu nyingine duniani na usimamizi madhubuti wa sera za fedha na bajeti.

Kuhusu uchumi wa Taifa hasa pato la Taifa Waziri Mwigulu amesema, licha ya mlipuko wa UVIKO-19 ulioathiri uchumi wa nchi nyingi ulimwenguni Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizokuwa na ukuaji chaja wa uchumi kwa mwaka 2020 huku uchumi ukitarajiwa kuimarika kufikia asilimia 4.4 ifikapo 2022 kutokana na matarajio ya kurejea kwa shughuli za kiuchumi.

"Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 kwa mwaka 2019, ukuaji chanya ulitokana na hatua ya Serikali ya kuruhusu shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea na wakati huohuo wananchi wakisisitizwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

"Aidha kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini kulichangiwa na athari za UVIKO-19 katika nchi washirika wa kibiashara pamoja na mafuriko yaliyosababisha uharibifu wa miundombinu ya usafirishaji na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo,"amesema.

Aidha amesema kuwa, athari za janga la UVIKO-19 zilijitokeza zaidi katika shughuli za kiuchumi za malazi, huduma ya chakula pamoja na sanaa na burudani ambazo zilikuwa na ukuaji hasi kwa mwaka 2020.

"Sekta zilizokua kwa viwango vya juu kwa mwaka 2020 ni pamoja na sekta ya ujenzi (asilimia 9.1,) habari na Mawasiliano (asilimia 8.4,) uchukuzi na uhifadhi wa mizigo (asilimia 8.4,) huduma zinazohusiana na Utawala (asilimia 7.8,) shughuli za kitaalamu, Sayansi na Ufundi (asilimia 7.3,) madini na mawe (asilimia 6.7,) pamoja na afya na huduma za jamii kwa asilimia 6.5," ameeleza.

Pia ameeleza kuwa, pato la Taifa ghafi lililozalishwa nchini lilikuwa ni shilingi trilioni 148.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na shilingi trilioni 139.6 mwaka 2019 huku idadi ya watu kwa mwaka 2020 Tanzania bara ilikadiriwa kufikia watu milioni 55.9 ikilinganishwa na watu milioni 54.2 kwa mwaka 2019 ambapo wastani wa pato kwa mtu lilikadiriwa kufikia shilingi 2,653,790 sawa na dola za kimarekani 1,151.0 kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na shilingi 2,573,324 sawa na dola za kimarekani 1,118.9 kwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1.

Kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha 2021/2022 Waziri Nchemba amesema, malengo ya utekelezaji wa fedha yalikuwa ni pamoja na kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi 40, ukuaji wa wastani wa fedha taslimu usiozidi asilimia 9.0, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi usiozidi asilimia 13.5 pamoja na ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) usiozidi asilimia 10.0.

Mwigulu amesema, Serikali kupitia benki kuu imeendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya fedha ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza baadhi ya viwango vya riba katika masoko ya fedha hususani riba za mikopo.
Waziri wa Fedha na Mipnago Mhe.Dkt.Mwigulu Nche,ba akiwasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi na Taifa kwa mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22.

No comments: