Jaji Mwangesi: Viongozi zingatieni Uadilifu


Kamishna wa Maadili Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi (kushoto) akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela ofisini kwa Mkuu wa Mkoa jijini ARusha wakati wa ziara yake Mkoani hum oleo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela akifungua kikao cha Viongozi wa Umma wa Mkoa wa Arusha kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo leo jijini Arusha. Kulia kwake ni Kamishna wa Maadili Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi na kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihamia.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi akitoa mada katika kikao cha Viongozi wa Mkoa wa Arusha kilichofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo

VIONGOZI wa Umma wametakiwa kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ilii waweze kuaminika na kukubalika katika jamii inayowazunguka.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi ametoa wito huo leo jijini Arusha wakati akitoa mada kuhusu maadili kwa viongozi wa umma katika kikao cha Viongozi wa Mkoa wa Arusha.

Mhe. Mwangesi amesema kuwa “Ni ukweli usiopingika kwamba viongozi waadilifu wanakubalika katika jamii na ni chachu kwa wananchi kuiga mifano ya uadilifu kutoka kwa viongozi wao.”

Kwa mujibu wa Jaji Mwangesi, Kiongozi wa Umma anapaswa kujipambanua kwa watu anaowaongoza kwa kutimiza wajibu wake bila kushurutishwa, pia anatumia uwezo na ushawishi alio nao kujenga uadilifu katika jamii.

Aidha Kamishna wa Maadili amesisitiza kuwa, kiongozi yeyote wa umma anapaswa kuwa na tabia na mwenendo usio kuwa na mashaka ili wananchi wamwamini na kuiamini Serikali anayoitumikia.

Katika hatua nyingine Jaji Mwangesi amewakumbusha viongozi kuzingatia misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayomtaka kila Kiongozi kuzingatia Maadili katika utekelezaji wa majukumu yake, Kuepuka mwenendo unaohaibisha utumishi wa umma baada ya kuacha wadhifa husika; hususani kujiepusha na tabia za ulevi, uhuni, kujihusisha na biashara zisizohalali.

“Katika kuzingatia misingi hiyo viongozi wanalazimika kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na miongozo katika kutekeleza majukumu yao,”amesema.

Misingi ya maadili inayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa uaminifu, huruma, umakini, kujizuia na tamaa na kuzingatia viwango vya juu vya maadili kadri iwezekanavyo. Misingi mingine ni kuzingatia haki, kutopendelea na kutenda kazi kwa uadilifu wa hali ya juu ili kulinda na kuimarisha imani ya wananchi na serikali.

“Jiepusheni na migongano ya kimaslahi kwani hairuhusiwi kufanya jambo au kutoa uamuzi kwa kuzingatia maslahi binafsi. Epukeni kuzingatia maslahi ya familia zenu au mtu mwingine yeyote mliye na uhusiano naye,” amesisitiza.

Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela amesema kuwa ipo changamoto kwa baadhi ya Viongozi wa Umma kudhani kuwa maadili yanahusika na ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na madeni tu.

Mhe. Mongela amefafanua kuwa Viongozi wengi wanatimiza tu kipengele cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinachowataka kakujaza Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kiloa ifikapo mwishoni mwa mwaka, lakini mienendo yao sio mizuri na hairidhishi kwani baadhi ya viongozi ni walevi, watoro, watumiaji wa lugha isiyofaa, wezi wa mali za umma na tabia nyingine nyingi zinazoipa taswira mbaya dhana ya uongozi.

“Viongozi wa Umma tunatakiwa kuwa na madili mazuri yasiyotiliwa shaka na kuyaishi yale tunayopaswa kuzingatia kwani kiongozi yeyote katika ngazi au wadhifa wowote ni kioo cha jamii husika,” amesema.

Kikao hicho cha Kamishna wa Maadili na Viongozi wa Umma ni sehemu ya Maadhjimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2021 ambapo Mhe. Mwangesi anatembelea wadau wa maadili, kutoa elimu na kusikiliza kero na malalamikoo yao kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

No comments: