WAZIRI AWESO: WAHANDISI CHEZENI NA VITAMBI VYENU SIYO MIRADI YA MAJI

     
Kamati ya Kidumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji chini ya Mwenyekiti wake, Christina Shengoma wakikagua mradi wa Maji wa Bugiri Chamwino mkoani Dodoma leo walipoambatana na Viongozi wa Wizara ya Maji chini ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (katikati) akiwa na baadhi ya Wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji walipotembelea mradi mkubwa wa maji Bugiri Chamwino leo.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji sambamba na viongozi kutoka Wizara ya Maji wakiongozwa na Waziri wake, Jumaa Aweso wakikagua mradi wa maji wa Mzakwe jijini Dodoma leo.


Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewaonya wahandisi na wakandarasi watakaochezea miradi ya Maji nchini ambapo amesema hatokubali kuona mtu yeyoye anakwamisha mpango na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama Ndoo kichwani.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maji katika Mkoa wa Dodoma iliyofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambapo Kamati hiyo imeeleza kufurahishwa na kuridhishwa na hatua zinazofanywa na Wizara ya Maji katika kutatua changamoto za maji mkoani hapa.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Aweso amesema kama kuna Mhandisi yeyote nchini anataka kucheza basi acheze na ndevu na kitambi chake na wala siyo miradi ya maji kwani serikali ya awamu ya sita ina mpango kabambe wa kumaliza changamoto ya maji na kumtua Mama Ndoo kichwani.

Aweso amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia Sh Bilioni Tano kwa ajili ya miradi ya maji mkoani Dodoma huku akieleza hadi sasa tayari washachimba visima 10, vitatu kati ya hivyo vikiwa ni vikubwa na kimoja kitakua na uwezo wa kuchukua Lita Laki Nne kwa saa.

" Kwanza niishukuru Kamati yetu ya kudumu ya Bunge kwa kutembelea na kukagua miradi yetu, niwatoe hofu serikali kupitia Wizara yetu ya Maji tunashughulikia kwa karibu changamoto ya  maji Mkoa wa Dodoma na tayari tumeshaanza mikakati ya kuvuta Maji kutoka Ziwa Viktoria ambapo tunaamini na Bwawa letu la Farkwa likikamilika basi shida itakua imeisha Dodoma," Amesema Waziri Aweso.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Christina Shengoma ameipongeza Wizara hiyo kwa namna ambavyo imejikita kumaliza changamoto ya Maji Mkoa wa Dodoma kupitia miradi yake ya Mzakwe jijini Dodoma na Bugiri Chamwino lakini akaitaka Wizara hiyo kuhamasisha wananchi kuvuna maji kupitia paa za nyumba.

" Changamoto hii ya maji Dodoma pia inasababishwa na wingi wa watu kuongezeka, kama Kamati tumeridhika na hatua ambazo Wizara inazichukua katika kuwahudumia wananchi wetu na tunaamini kukamilika kwa mradi wa kuleta Maji kutoka Ziwa Viktoria kutachangia kumaliza kero ya maji," Amesema Mwenyekiti huyo.

No comments: