WANAOVUNA MITI SHAMBA LA SHUME WATAKIWA KUVUNA META ZA UJAZO WALIZOPEWA KUVUNA 2020/2021






 Na Tulizo Kilaga,TFS

SERIKALI imewataka wafanyabiashara wanaovuna miti katika Shamba la Miti Shume kuhakikisha wanalipia na kuvuna meta za ujazo walizopewa kwa ajili ya kuvuna katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 kabla migao hiyo kugaiwa watu wengine.

 Akizungumza katika mkutano wa wafanyabishara hao uliondaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Naibu Kamishna wa Uhifadhi TFS Mohamed Kilongo amesema ikiwa imebaki miezi miwili ili mwaka wa fedha kuisha, Serikali imeona ni vema ikakutana na wafanyabiashara na wananchi inayowahudumia kuzibaini changamoto zao na kutafuta namna ya kuzitatua ili kuongeza kasi ya uvunaji.

 "Tumekuja hapa kuwasikiliza ni nini ambacho tunatakiwa kukiongeza zaidi ili tuweze kuvuna kwa kasi! Hadi sasa uvunaji uko asilimia 48 huku ikiwa tumebakiza miezi miwili tu tufunge zoezi la uvunaji katika mwaka huu wa fedha, uvunaji uko chini na una adhali kubwa kwa pande zote mbili za wafanyabiashara na Serikali,"amesema.

Amefafanua adhali hizo kuwa, kwa upande wa wafanyabiashara licha ya kupewa mgao huo hawajafanya biashara huku upande wa pili wa Serikali ukishindwa kufikia lengo la makusanyo na hivyo kukwamisha miradi ya maendeleo na matumizi mengine ya Serikali kwa sababu ya wafanyabiashara hao kushindwa kulipa na kuvuna miti waliyoomba kuvuna.

 Naibu Kamishna Kilongo anasema anajua kwa sasa soko la mbao limekuwa gumu kwa wavunaji wa mashamba ya miti ya serikali kutokana na soko la mbao changa kushika kasi kwenye soko la ndani huku lile la nje likikwamishwa na Covid 19.

 "Ninafahamu kwa sasa bei ya mbao zinazozalishwa na miti michanga sokoni iko chini ukilinganisha na mbao zinazozalishwa kwenye miti bora iliyokomaa ya Serikali, suala hili tunalishughulikia ili Watanzania waweze kupata bidhaa bora, lakini niwataka nanyi mnapotafuta masoko msisitize suala la ubora, huwezi kuta mbao yetu imebunguliwa ndani ya muda mfupi kama ilivyo kwa zile zisizo na ubora,"amesisitiza.

Ameongeza pamoja na changamoto hiyo wapo wafanyabiashara waliomaliza kuvuna meta za ujazo walizoomba lakini wanashindwa kupewa mgao mwingine kutokana na wengine kuendelea kushikilia migao yao licha ya kushindwa kuvuna, na hivyo kumuagiza mhifadhi wa shamba la miti Shume kuhakikisha anawabana wale wote walioshindwa na kuwapa wale wenye uhitaji.

Kwa upande wake Mhifadhi wa Shamba la Miti Shume, Ernest Madata alisema kwa kutambua kuwa msimu wa uvunaji unaelekea ukingoni alifanya kibao na wavunaji hao wiki iliyopita na kukubaliana ifikapo Jumatatu, Mei 03, 2021 wafike ofisini na kusema katika kipindi cha mwezi mmoja uliobaki kiasi gani wanaweza kuvuna ili taratibu zingine ziweze kufanyika.

 "Kwa sababu tunaelekea ukingoni mwa msimu wa uvunaji wa mwaka wa fedha 2020/2021 na kuna wateja ambao wako chini sana, tulikaa kikao na kukubaliana kwamba Jumatatu waje waseme katika migao yao ni kiasi gani wanaweza kuliupia na kuvuna katika kipindi cha mwezi mmoja uliobaki ili kiasi kinachobaki kiweze kutolewa kwa wavunaji wenye uhitaji kuliko kuendelea kuikosesha Serikali mapato,"amesema Madata

 Ally Masoud ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wanaovuna katika shamba hilo aliyemaliza mgao wake anasema anashukuru kwa uamuzi huo utakaomuwezesha kukamilisha oda za wateja wake na kuwataka wafanyabishara wenzake kushirikiana katika kuonyeshana fursa za masoko.

No comments: