WANAONYONYESHA WAOMBA MAREKEBISHO SHERIA YA LIKIZO

Mama akiwanyonyesha watoto wake mapacha  huku akiwa anafurahia na kutafakari jambo lake moyoni. 


Na Abby Nkungu, Singida

WAKATI leo dunia inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama “Mei Mosi”, wanawake waliopo kwenye utumishi wa umma na sekta binafsi wameiomba Serikali kuvifanyia marekebisho baadhi ya vipengele vya Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini ili  kutoa  haki na kukidhi mahitaji ya  kiafya kwa malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.

Wakizungumza na Mwandishi wa Blog hii kwa nyakati tofauti, baadhi yao walisema kuwa Sheria hiyo  imekuwa kikwazo  katika utekelezaji wa  miongozo, kanuni na taratibu nyingine za kiafya;  hivyo kuathiri suala zima la malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.

Walisema kuwa wakati miongozo ya afya inataka mtoto mchanga anyonyeshwe  maziwa ya mama pekee  kwa miezi sita mfululizo bila kumchanganyia chakula kingine, Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini inatoa siku 84 tu za likizo ya uzazi ambazo hazizidi miezi mitatu na ni hatari kiafya kwa mtoto mchanga.

“Hebu fikiria Serikali hiyo hiyo kupitia Wizara ya Afya inatutaka tunyonyeshe miezi sita mfulilizo halafu Utumishi wanatupa likizo ya miezi  mitatu tu, hii sio sawa. Ni kumnyima haki mtoto na mzazi wake lakini pia  inaweza kuathiri makuzi ya mtoto” alisema Halima John  mkazi  wa Mwenge  mjini Singida.

Neema Omari,  mkazi wa Ginnery mjini hapa alisema kutokana na siku za likizo kuwa chache huwa wanalazimika kukamua maziwa  yao na kuyahifadhi kwenye chupa ya chai ili mtoto aweze kupewa na yaya au mtu mwingine anayebaki nyumbani pindi yeye awapo kazini.

Kaimu  Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Ernest Mugeta alisema kuwa ingawa  mtindo huo umezoeleka kwa akinamama watumishi wanaonyonyesha, njia hiyo sio sahihi kwani mbali na maziwa hayo kupungukiwa baadhi ya virutubisho yanapohamishwa kutoka kwa mama kwenda kwenye chombo kingine pia inatenganisha mahusiano mema baina  ya mama na mtoto.

“Usafi wa maziwa hayo baada ya kutoka kwenye titi la mama ni wa kutiliwa shaka. Pia, joto na ladha ya maziwa yanayotoka moja kwa moja kwenye titi la mama kwenda kwa mtoto haiwezi kulinganishwa na joto la chombo chochote cha kuhifadhia maziwa hayo… iwe chupa ya chai au vinginevyo” alieleza Dk Mugeta na kuongeza;

Kimsingi, uhusiano wa karibu wa mama na mtoto hutokana na mtoto kunyosha titi la mama, anazoea harufu ya mama na ndio maana mtoto humjua mama zaidi kuliko baba. Hivyo, inashauriwa pale inapowezekana mama apewe ruhusa ya kwenda kunyonyesha hata baada ya likizo yake ya uzazi kumalizika”.

Kutokana na hali hiyo, akinamama walisema kuwa kuna haja kwa Serikali kuvifanyia marekebisho baadhi ya vipengele vya Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini  ili kutoa muda zaidi wa likizo kwani kumruhusu mama mzazi kwenda nyumbani kunyonyesha kisha kurudi kazini inaleta usumbufu na haitekelezeki mahali pengine kama Dar es Salaam.

Kwa Mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Namba 6 ya mwaka 2004, mtumishi hupewa siku 84 za  likizo kwa anayejifungua mtoto mmoja, siku 100 kwa anayejifungua mapacha na siku tatu kwa baba wa mtoto huyo.

Ofisa Kazi Mfawidhi mkoa wa Singida, Bibi Eunice Mmari anasisitiza kuwa likizo hiyo inatosha kwa mama kumlea mtoto na kuweka mazingira mazuri ya usalama na ulinzi wake baada ya  yeye kuanza kazi likizo inapomalizika; hiyo ikizingatia pia kutoathiri tija mahali pa kazi.

No comments: