WANANCHI WAASWA KUZINGATIA UTUNZAJI SAHIHI WA NOTI

 

Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki BoT, Victoria Msina, akiwafundisha wananchi alama za usalama zilizopo katika noti zetu kwenye soko la Munanila wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Afisa Mkuu Mwandamizi wa Benki BoT, Bw. Francis Mdoe, akifafanua jambo kwa mwananchi kuhusu alama za usalama zilizopo katika noti zetu kwenye soko la Munanila wilayani Buhigwe mkoani Kigoma.

Wananchi kwenye soko la Munanila wilayani Buhigwe mkoani Kigoma wakijadiliana kuhusu alama za usalama katika noti.

Wananchi kwenye soko la Munanila wilayani Buhigwe mkoani Kigoma wakipewa vipeperushi vyenye maelezo kuhusu alama za usalama katika noti zetu.

Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki BoT, Victoria Msina akiwaelekeza wafanyabiashara namna ya kutumia taa ya rangi ya zambarau kuangalia alama za usalama zilizofichika katika noti zetu.

Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki BoT, Victoria Msina akimuelekeza Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Kigoma, Dkt. Vedast Makota, alama za usalama zinazoweza kuonekana kwa kupapasa noti kwa vidole.

Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki BoT, Victoria Msina akitoa elimu kwa wafanyabiashara na maafisa wa serikali mkoani Kigoma kuhusu namna ya kutambua alama za usalama katika noti zetu.

Afisa Mkuu Mwandamizi wa Benki BoT, Bw. Francis Mdoe, akieleza kuhusu haki na wajibu wa mteja anapofanya miamala ya fedha taslimu katika benki za biashara kwa wafanyabiashara na maafisa wa serikali waliohudhuria semina ya alama za usalama katika noti iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma.

Afisa Mkuu Mwandamizi wa Benki BoT, Bw. Francis Mdoe, akigawa vipeperushi kwa wafanyabiashara na maafisa wa serikali waliohudhuria semina ya alama za usalama katika noti iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma.

………………………………………………………………………………………..

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imewaasa wananchi mkoani Kigoma kuzingatia utunzaji sahihi wa noti na sarafu katika shughuli zao za kila siku ili kupunguza ongezeko la noti chakavu katika mzunguko. 

Akizungumza na wakulima na wafanyabiashara katika soko la Munanila wilayani Buhigwe, Meneja Msaidizi Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Victoria Msina, amesema kuwa utunzaji sahihi wa noti na sarafu unasaidia kupunguza gharama kubwa ambazo serikali inatumia kuchapisha noti upya ili kufidia zile zilizoharibika. 

Alitaja baadhi ya vitendo vya utunzaji mbaya wa noti na sarafu kuwa ni pamoja na kukunja au kufinyanga noti mkononi, kuweka noti/sarafu katika soksi mguuni au chini ya godoro, kuweka fedha sehemu zenye uchafu au unyevunyevu, kuweka noti kwenye nguo za ndani au kuzifunga kwenye kona ya kanga au kitenge pamoja na kuzichimbia ardhini. 

“Ili kuhakikisha ubora wa noti na sarafu unadumu kwa kipindi kirefu, mwananchi yeyote anayepokea noti au sarafu, anatakiwa kuzihifadhi pesa hizo katika pochi ya kuhifadhia fedha ili zisipate mikunjo na uchafu,” alisema. 

Aliongeza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kuwa na pochi imara za mifukoni au makasha ya kuhifadhia fedha ili zisichafuke, kujikunja au kuchanika. 

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha fedha zinahifadhiwa sehemu safi zisizo na unyevunyevu, vumbi, kemikali, rangi au vyombo vinavyotoa rangi. Vilevile, zihifadhiwe mahali salama pasipofikika na moto, maji, wadudu na wanyama. 

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mwandamizi wa BoT, Bw. Francis Mdoe, alisema kuwa wateja wote wa benki za biashara, wana haki kupewa noti safi kutoka katika kaunta za benki na katika mashine za kutolea fedha (ATM) pamoja na kupewa chenji katika sarafu na noti za thamani yoyote kupitia utaratibu wa kutoa fedha kutoka katika amana zao.

 

Akizungumzia alama za usalama katika noti, Bw. Mdoe alisema kuwa wananchi wanapaswa kujua alama hizo ili kuwawezesha kutambua noti halali na kuwasaidia kuepuka utapeli. Aliwahimiza wananchi kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo karibu pindi wanapopokea au kupata taarifa kuhusu kuwepo kwa noti bandia. 

Benki Kuu ya Tanzania inaendesha kampeni ya elimu kwa umma kuanzia tarehe 17 hadi 21 Mei, 2021 mkoani Kigoma, inayolenga makundi mbalimbali ya wananchi kwa lengo la kuwaongezea ufahamu kuhusu alama za usalama katika noti zetu na namna sahihi ya utunzaji wa noti na sarafu.

No comments: