WAFANYABIASHARA, VIJANA NA WANAWAKE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIMAENDELEO ZA JUMUIYA YA SADC
Na Charles James, Michuzi TV
TAASISI za Elimu nchini,Wafanyabiashara na Vijana wameaswa kuchangamkia iliyopo kwenye Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.
Kauli hiyo imetolewa leo na Meya wa Jiji la Dodoma, Prof Davis Mwamfupe wakati akifungua kongamano la kujadili miaka 40 ya Jumuiya hiyo ya SADC katika eneo la Ujenzi wa Amani na Usalama,Ukuaji wa Maendeleo na uhimilivu katika kukabiliana na changamoto zake.
Prof Mwamfupe amesema mkutano huo wa miaka 40 ya SADC mbali na kueleza faida zake lakini pia utumike kuongeza hamasa kwa makundi ya wafanyabiashara, vijana na Wanawake katika kuchangamkia fursa za kimaendeleo zilizopo katika Nchi wanachama.
" Inatupasa tuenende na mabadiliko ya kiteknolojia Leo tunapoadhimisha miaka 40 ya SADC, pamoja na kutumia mkutano huu kuwaenzi waasisi wa Jumuiya hii Mwl Julius Nyerere na wenzake lakini pia tuwaeleze watanzania namna wanavyoweza kuchangamkia fursa katika Nchi wanachama kama Angola, Zambia au Afrika Kusini.
Niwapongeze Chuo Kikuu Cha Dodoma na Chuo Cha Diplomasia pale Dar es Salaam kwa kutambua fursa za kielimu kwani nafahamu mna wanafunzi kutoka mataifa mengine wanachama ya SADC, nizisihii taasisi zingine za Elimu kuchangamkia fursa hii," Amesema Prof Mwamfupe.
Amesema ukizungumzia mafanikio ya Jumuiya ya SADC huwezi kukwepa kutambua mchango Mkubwa wa Tanzania katika kuanzisha na kukuza Jumuiya hiyo na hasa mchango wa Baba wa Taifa Mwl Nyerere.
" Kwa miaka ya hivi karibuni hapana shaka mchango wa aliyekua Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Dk John Magufuli alifanya kazi kubwa alipokua Mwenyekiti wa mkutano wa 39 wa SADC.
Akiwa Mwenyekiti amesaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwenye Nchi za SADC lakini kubwa zaidi Ni kuchochea kuridhiwa kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za SADC," Amesema Prof Mwamfupe.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Cha UDOM, Prof Faustine Bee ameshukuru Chuo hicho kupata nafasi ya kuandaa kongamano hilo huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoendeleza mahusiano ya kimataifa.
" Sisi UDOM ni wanufaika wakubwa wa Nchi yetu ya Tanzania kuwa mwanachama wa SADC kwani tunapokea wanafunzi kutoka Nchi wanachama ikiwemo DR Congo, Burundi, Afrika Kusini, Msumbiji na hata Visiwa vya Comoro.
Na moja ya malengo yetu ni kuingia katika idadi ya Vyuo 20 bora barani Afrika kufikia mwaka 2030 na hilo litawezekana kwa kuongeza pia idadi ya wanafunzi kutoka Nchi zingine wanaosoma hapa kwetu," Amesema Prof Bee.
No comments: