Wadau wa chai wakoshwa na usimamizi wa mashamba,waomba mamlaka kuwasaidia wakulima mashine

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Katika kuhakikisha wakulima hapa nchini wanapata masoko ndani na nje ya nchi kutokana na ubora wamepatiwa mafunzo yatakayowawezesha kupata vyeti vya ubora wa kimataifa watakavyotumia katika masoko ya mazao yao.

Mara baada ya mafunzo ya IMS yenye lengo la kuwajengea uwezo wa uendeshaji wa mifumo ya kisasa katika viwanda na makampuni ya chai kwenye semina ya siku Mbili chini ya mradi wa Mark Up kwa ufadhiri wa umoja wa ulaya wadau mbali mbali kutoka maeneo ya wazalishaji wa Chai Tanzania wamefika na kujifunza kwa vitendo uendeshaji wa mashamba ya wananchi wa Lwangu.

Akieleza umuhimu wa mafunzo hayo baada ya kutembelea mashamba ya chai ya Nosci mshauri wa mradi huo kutoka Markup Christian Sakalani amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wakulima kupata bidhaa itakayoendana na mahitaji ya soko la kimataifa.

Alisema duniani kwasasa kumekuwa na uhitaji makubwa wa mtumiaji wa zao au bidhaa kutaka kufahamu namna lilivyozalishwa ndipo ukaja mfumo wa kuthibitisha ubora wake kwa njia ya vyeti.

Alisema mfumo huo umeanzishwa ili mtumiaji wa bidhaa aweze kufahamu utunzaji na uzalishaji wa bidhaa husika ulivyozingatia mazingira yanayohitajika kwenye zao husika.

"ITC walikuja na program hii baada ya kuona baadhi ya makampuni yanafanya uthibitishaji wa vyeti mbalimbali na kila cheti kilikuwa na mahitaji yake" alisema Sakalani.

"ITC wakaja na lengo la kuhakikisha kuna mfumo mmoja utakaowezesha chama au kampuni iweze kutumia huo mfumo kupata certification scheme ya aina yoyote" aliongeza Sakalani.

Alisema vyeti hivyo ni muhimu kwakuwa vinaweza kuwasaidia wakulima na wamiliki wa viwanda kuingia katika soko la viwango vya juu kutokana na mfumo huo.

Meneja muendeshaji wa kampuni ya Nosci Haidari Nawabu alisema katika kuwawezesha wakulima wa zao la chai mkoani Njombe wamekuwa wakitoa huduma za ugani na kuwapa mkopo wa pembejeo usiokuwa na riba.

Alisema pia wamekuwa wakiwapatia wakulima dawa za kuua magugu huku wakizalisha miche na kuwapatia wakulima wenye mashamba mapya.

Alisema wana wakulima wanaozalisha ambao wana  vyeti vya ubora wa zao la chai wapatao 1770 ambapo zoezi hilo wamelifanya kuwa endelevu kwakuwa kila mwaka kuna wakulima wanaowathibitisha kwa ubora na kuwapa vyeti.

"Achana na wale ambao wanatakiwa kuhuwisha vyeti vyao ni kwamba unakuwa na mkulima mpya ambaye ameanzisha shamba jipya" alisema Nawabu.

Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa chai cha mshikamano kilichopo Lwangu mkoani Njombe  Blasius Menlufu alisema zao la chai ni la muda mrefu na la biashara ambalo lina faida kubwa.

Alisema miongoni mwa changamoto inayowakabili ni upatikanaji wa mashine zinazotumika kuchuma chai ili kukidhi ubora wake kwenye soko la kimataifa.

"Ukichuma kwa mikono inasababisha kuchelewa na kupunguza ubora wa chai mfano kama ulikuwa uchume chai kwa kipindi cha siku saba unatumia siku kumi" alisema Blasius.

Aidha wadau waliowatembelea wakulima hao wameziomba mamlaka za usimamizi ikiwemo NOSC na Serikali kuwasaidia wakulima hao nyenzo za uchumaji chai ili kurahisisha zoezi la uchumaji majani.

Aidha wameipongeza Serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa chai wanaoendelea kujitolea katika kumsaidia mkulima na kufikia kilimo endelevu.
Baadhi ya wadau waliokuwa katika mafunzo wakiwa katika ofisi za kampuni ya NOSC inayowasaidia wakulima wakipata maelezo namna kampuni hiyo inayowasaidia wakulima.

Wadau wa chai wakipata maelezo walipotembelea wakulima wa kikundi cha mshikamano kilichopo Lwangu mkoani Njombe.
Wakulima wa chai wa kikundi cha mshikamano wakichambu majani ya chai

No comments: