RUZUKU YA BILIONI SABA YATOLEWA KWA VIJANA KUJIKIMU NA KUANZISHA BIASHARA
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mwitikio wa Kitaifa kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Audrey Njelekela, akizungumza katika kikao kazi wakati wa kuutambulisha Mradi wa Awamu ya Pili wa Timiza Malengo (AGYW) mjini hapa jana.
Afisa Elimu Taaluma Mkoa wa Singida, Ayoub Mchana, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mratibu wa TASAF Mkoa wa Singida, Patrick Kasango akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Picha ya pamoja na Mgeni Rasmi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick, (katikati waliokaa)
Na Dotto Mwaibale, Singida
JUMLA ya Sh. 7,442,100,000 zimetumika kwa Wasichana Balehe na wanawake Vijana walio ndani ya shule wapatao 16,011 na jumla ya walengwa 9,971 walio kuwa nje ya shule kwenye mradi wa Timiza Malengo (AGYW) kwa Awamu ya Kwanza walipatiwa ruzuku ya kujikimu na kuanzisha biashara.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mradi huo kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) , Edgar Mapunda wakati akizungumzia mafanikio ya mradi huo Awamu ya Kwanza ulioanza kwa majaribio Mwaka 2018 hadi Desemba 2020 na kuutambulisha mradi wa Awamu ya Pili katika kikao kazi kilichofanyika mjini hapa jana.
Mapunda alisema Sh. 3,888,430,333.00 zilitumika kwa Wasichana Balehe 9971 walio kuwa nje ya shule kwa ajili ya mitaji ya kuanzisha biashara.
" Mafanikio mengine yaliyopatikana ni kuongeza hamasa na kuimarisha mikakati ya kuwafikia Wasichana Balehe na Wanawake Vijana walio ndani ya shule 16,011 katika Halmashauri na Mikoa iliyoanishwa Kitaifa." alisema Mapunda.
Alisema Vijana 47,705 walifikiwa na kampeni ya kipepeo na inakadiriwa kuwafikia vijana zaidi ya 8,630,161 kupitia redio.
Aidha Mapunda alisema Wazazi wapatao 10,470 walipatiwa mafunzo ya malezi na makuzi, viongozi 1,114 waliemishwa kuhusiana na mila na desturi zinazoweza kusababisha maambukizi ya VVU na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi.
" Inakadiriwa takribani Wasichana Balehe na Wanawake Vijana 200,000 walipata habari kupitia radio za kijamii kupitia vipindi 15 vilivyoandaliwa" alisema.
Akitaja mafanikio zaidi Mapunda alisema jumla ya kondomu ‘dispenser’ zipatazo 5,000 zilinunuliwa na kusimikwa kwenye maeneo hatarishi na maeneo ya kazi na Vijana balehe 165,497 walipatiwa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya VVU na UKIMWI huku Wasichana Balehe na Wanawake Vijana 148,002 walifikiwa na huduma za upimaji wa VVU ambapo kati yao 3,191 waligundulika kuwa na maambukizi na jumla ya 2,873 walianzishiwa huduma za tiba.
Alitaja baadhi ya changamoto kwenye Awamu ya Kwanza kuwa ni upungufu wa elimu ya VVU na UKIMWI, Afya ya Uzazi na stadi za maisha mashuleni, Upungufu wa mifumo,Madhubuti wa ufuatiliaji kwa ngazi ya mlengwa pamoja na upungufu wa huduma Rafiki kwa vijana katika vituo vya afya na mafunzo kwa wafanyakazi Mikakati Madhubuti ya kushughulikia masuala ya Ukatili wa kijinsia Wanaume wengi kutojitokeza kupata huduma.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni ucheleweshwaji wa uhaulishaji fedha kwa walengwa wakati wa kipindi cha mpito kwenye mradi wa TASAF kutoka TASAF I kwenda TASAF II.
Awamu ya Pili ya mradi huo utatekelezwa katika maeneo ya Morogoro (Mlimba DC, Ifakara TC, Morogoro MC, Ulanga DC na Malinyi DC) na Dodoma (Kongwa DC, Mpwapwa DC, Chamwino DC, Kondoa TC , Dodoma MC, na Bahi DC) Singida ni (Iramba DC, Singida MC na Singida DC), Geita (Geita DC and Chato DC)Tanga (Tanga MC).
Mradi huo unatekelezwa kwa ufadhili wa Global Fund kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, TAMISEMI, Amref Health Africa pamoja na Taasisi ya Vijana Tanzania (TAYOA).
No comments: