NAIBU WAZIRI GEKUL AIPONGEZA SIMBA QUEENS

 Na Mwandishi wetu, Dodoma


NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mhe Pauline Philip Gekul ameipongeza timu ya soka ya wanawake ya Simba Queens  kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya wanawake (Serengeti Lite Women Premier League).

Mhe Gekul akizungumza jijini Dodoma leo Jumatatu Mei 17 wakati timu hiyo ilipotembelea Bungeni amesema Simba Queens imestahili kushinda ubingwa huo kutokana na namna ilivyokuwa inapambana uwanjani kwenye michezo yake.

"Nina wapongeza viongozi, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wote kwa juhudi kubwa mlizoonyesha katika kipindi chote cha ligi na kuweza kuwa mabingwa kwa mara ya pili mfululizo," amesema mhe Gekul.

"Ligi ilikuwa na ushindani mkubwa lakini mmeweza kuibuka washindi, hii ni ishara kuwa ligi yetu ya wanawake inazidi kuimarika,"  amesema mhe Gekul.

Timu ya Simba Queens imepata mwaliko maalumu wa kutembelea bungeni leo tarehe 17 Mei, 2021 mara baada ya kutwaa taji la ligi ya wanawake kwa kuifunga timu ya Baobab Queens goli 1-0 katika mchezo uliofanyika jana kwenye uwanja wa jamhuri jijini Dodoma.

 

No comments: