NAIBU WAZIRI AAGIZA TAASISI YA MAENDELEO YA JAMII KUJITANGAZA
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis ameziagiza Taasisi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kujitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kuwawezesha wananchi kunufaika na Huduma za vyuo hivyo.
Naibu Waziri Mwanaidi ametoa agizo hilo Jijini Arusha mara baada ya kufanya ziara katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa lengo la kukagua Maendeleo ya miradi ya Ujenzi chuoni hapo.
Amesema pamoja na ongezeko la udahiri wa wanachuo, Taasisi inatakiwa kujitangaza na kusambaza taarifa zaidi kuhusu huduma na mafunzo yake kwa Jamii ili kuwezesha wanufaika wengi kupata ujuzi.
"Naomba niseme kwamba mnafanya kazi kubwa na nzuri kwa Jamii ya Watanzania, lakini bado Jamii inahitaji kupata taarifa zaidi na kwa kufanya hivyo, wananchi wataelimika, wataweza kujiajiri na kuajiri wengine" alisema Naibu Waziri Mwanaidi.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa mabweni na kumbi za mihadhara katika Taasisi hiyo, Mwanaidi amesema Serikali ameanza kutenga fedha kwa ajili hiyo na hivyo ni muhimu kusimamia matumizi yake.
"Shilingi Bilioni 2.7 zinazotarajiwa kutumika kwa ajili ya Ujenzi wa ni fedha nyingi hivyo ni muhimu kuzitumia kadri ilivyokusudiwa na mimi nitarudinkuhakikisha zimetumika kama ilivyolengwa" aliongeza.
Amefafanua kuwa hadi sasa tayari Sh Bilioni moja zimetolewa na Serikali kwa ajili ya Mabweni ya wanafunzi wa Kike na Ukumbi wa mihadhara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro amesema Taasisi hiyo ni muhimu sana kwani inatoa fursa kwa vijana kupata elimu kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuwasaidia vijana kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine.
Aidha ameishukuru Serikali kwa hatua ya kutoa shilingi Bilioni moja za Ujenzi na kuahidi kwamba Wilaya yake itashirikiana na Taasisi kutimiza azima ya Serikali katika kuona fedha za miradi zinafanya kazi iliyokusudiwa.
"Ni muhimu kujipanga sisi wenyewe na kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa bei za jumla kuwatumia wataalam wa ndani katika utaratibu wa ujenzi" alisema.
Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri, Mkuu wa Taasisi hiyo, Dkt. Bakari George amesema Taasisi hiyo inaongeza udahiri wa Wanafunzi Kutoka wanafunzi 1167 hadi wanafunzi 2,608 huku mpango ukiwa ni udahiri wa wanafunzi 5000.
Ameongeza kuwa uwepo wa Kituo cha ubunifu cha kidigitali kimesaidia kulea na kuatamia mawazo ubunifu ili wahitimu na watu wa maeneo jirani waweza kutumia fursa ya kujiajiri na kuwaajiri wengine.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis akipata maelezo ya Miradi ya ujenzi wa Mabweni ya Wasichana na Kumbi za Mihadhara kutoka kwa Naibu Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Utawala na Fedha Janeth Zemba wakati alipotembelea Taasisi hiyo.
No comments: