MZEE MWINYI KUONGOZA MATEMBEZI YA HISANI KUTAFUTA FEDHA YA CHANJO YA INI KWA AJILI YA WANAFUNZI 2000 MUHAS

Na Zainab Nyamka, Michuzi TV

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi anatarajiwa kuongoza matembezi ya hisani kwa lengo la kuchangisha fedha ambazo zitasaidia wanafunzi wa chuo hicho zaidi ya 2000 kupatiwa chanjo ya Ini ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Chuo hicho ni asilimia 2 tu ya wanafunzi 2600 ndio  wamefanikiwa kupata chanjo ya homa ya ini kutokana na changamoto ya kifedha na wengine kutokupata mkopo wa elimu ya juu.

Hivyo Baraza la Chuo sambamba na Serikali ya wanafunzi MUHASSO wameamua kwa pamoja kufanya matembezi ya hisani yatakayohusisha uchangiaji wa fedha zitakazosaidia wanafunzi kupata kinga ya homa ya ini Mei 30 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Dk.Harrison Mwakyembe amesema elimu ya afya na tiba imekuwa inapanuka kwa kiasi kikubwa  na kupelekea  serikali kubeba mzigo mkubwa  wa gharama.

Amesema kwa sasa chuo kina wanafunzi takribani 4300 na wote wanatakiwa kupata chanjo ya homa ya ini ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo kwa sababu ya kukutana na watu mbalimbali pindi wanapotoa huduma.

Dk.Mwakyembe amesema matembezi hayo yatakuwa ni endelevu na Rais Mstaafu wa awamu ya pili Alhaji  Ali Hassan Mwinyi ambaye ni Mkuu wa Chuo hicho atayaongoza kwa umbali wa kilomita 6 kuanzia Masaki hadi Chuo cha Muhimbili.

" Chanjo ya homa ya ini ni muhimu sana  kwa wanafunzi wa udaktari, uuguzi, ufamaisia na meno na hiyo ni kulingana na mazingira wanayokutana nayo," amesema.

Dk.Mwakyembe amesema," changamoto zipo kwani wanafunzi wengine wamekuwa hawapati mkopo wa elimu ya juu ambao ni asilimia 20.4 kwa mwaka 2020/21 na kushindwa kumuda gharama za chanjo"

Aidha amesema gharama za kupata chanjo ya homa ya ini haipo katika bima ya afya na baada ya  wazo la kufanya matembezi ya hisani ioi kuweza kuchangia kuletwa katika baraza la chuo lilipelekwa kwa Mkuu wa Chuo na kulipa baraka zote.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS  Profesa Andrea Pembe amewaomba  viongozi wa Serikali,asasi za kiraia, taasisi na wadau mbalimbali kushirikiana katika matembezi ya hisani na kuchangia ili kupata fedha za chanjo kwa wanafunzi hao.

Amesema gharama za chanjo hiyo kwa mtu mmoja ni Sh.40,000 na kiasi kinachohitajika ni sh.Milioni 120 na suala hili ni endelevu kwa wanafunzi wote waliopo katika Chuo hicho.

Wakati huo huo Rais wa Serikali ya wanafunzi MUHASO Benedict Msaki ameushukuru uongozi wa chuo kukubali kufanya matembezi ya hisani kuchangia mfuko wa chanjo ya homa ya ini.

Aidha, ameongezea na kusema matembezi hayo yatahusisha kuchangua fedha lakini ni afya na katika siku hiyo wanafunzi kwa umoja wao watachangia damu tukio litakalofanyika katika Viwanja vya Chuo hicho.

Wanafunzi wanaosomea fani mbalimbali za udaktari, uuguzi, ufamasia, meno na zingine wanahitajika kupata chanjo ya homa ya ini kutokana na kukutana na watu mbalimbali wakati wa utoaji huduma.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dkt Harrison Mwakyembe akizungumzia matembezi ya hisani ya kuchangia homa ya ini kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo cha MUHAS yatakayofanyika Mei 30 mwaka huu na kuongozwa na Mkuu wa Chuo Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Dkt Ali Hassan Mwinyi .

No comments: