Mabondia zaidi kupamba Rumble in Dar 2, Wadhamini wanena
Katika kuhakikisha kuwa mabondia wengi wanapata nafasi ya kuonesha vipaji vyao, kampuni ya Jackson Group Sports imewapa nafasi zaidi mabondia wa Tanzania mbali ya bondia Hassan Mwakinyo ambaye atazichapa na bondia wa Zimbabwe, Brendon Denes ambao watawania mkanda wa uzito wa super welter wa Afrika (ABU) kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Mei 28.
''Awali, pambano hilo lilikuwa lishirikishe mabondia watatu tu wa Tanzania ambao ni Mwakinyo, Ibrahim Class na Shaban Jongo, hata hivyo, jumla ya mabondia wanne zaidi'',alisema Afisa Mtendaji Mkuu wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa.
Alisema kuwa Mabondia hao ni Imani Daudi ambaye atazichapa na bondia wa Afrika Kusini Chris Thompson, Hamis Palasungulu ambaye atazichapa na Ardi Ndembo wa Congo Brazzaville na mwanadada Halima Bandola ambaye atazichapa na bondia wa Bulgaria Joana Nwamerue.
Pia katika orodha hiyo yupo Daniel Materu ambaye atazichapa na bondia Pencho Tsvetkov wa Bulgariaa.
Twissa amesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kukuza vipaji kwa mabondia wa Tanzania katika pambano hilo ambapo benki ya KCB imetangaza kudhamini pambano hilo kwa Sh 94.4 millioni.
Twissa amesema kuwa maandalizi ya pambano la raundi 12 linaendelea vizuri na mkanda huo kwa sasa upo wazi.
Alisema kuwa siku hiyo kutakuwa na mapambano mengine makali ambapo bondia Jongo Jongo naye atawania ubingwa wa ABU dhidi ya Olanrewaju Durodora wa Nigeria.
Pia bondia Ibrahim Class atapanda ulingoni kumsindikiza Mwakinyo kupambana na bondia Sibusiso Zingange kutoka Afrika Kusini.
“Hii ni sehemu ya pili ya Rumble In Dar na tunaitarajia kuwa kali na kusisimua kwani mabondia wanaopigana ni moto wa kuotea mbali,” alisema Twissa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki ya KCB Christine Manyenye alisema kuwa wameamua kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya pambano hili ili kuendeleza mchango wao katika maendeleo ya michezo nchini.
Manyenye alisema kuwa bendi yao pia inadhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mashindano ya Ndondo Cup na riadha ambapo ilidhamini mashindano ya Rock City marathon.
Kwa upande wake, Meneja Masoko wa M-Bet Tanzania, Allen Mushi amesema kuwa wameamua kuingia katika ngumi za kulipwa kwa lengo la kupanua wigo wa shughuli zao.
Mushi alisema kuwa M-Bet kwa sasa inadhamini timu ya Ligi Kuu ya KMC na wanajisikia fahari kubwa kudhamini ngumi za kulipwa kwani ni mchezo namba mbili hapa nchini.
Mkuu wa Masoko wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo alisema kuwa pambano hilo linatarajia kuonekana katika zaidi ya nchi 32 za Afrika na nchi mbalimbali duniani kupitia DStv app.
Shelukindo alisema kuwa pambano hilo litaonekana kwenye chaneli ya Plus TV ambayo ipo kwenye king’amuzi cha DStv na kuwaomba mashabiki wa ngumi za kulipwa kujiunga nacho. Pambano hilo pia limedhaminiwa na Onomo Hotel na Clouds Media Group.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa pichani kati akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Mpambano wa Hassan Mwakinyo ambaye atazichapa na bondia wa Zimbabwe, Brendon Denes ambao watawania mkanda wa uzito wa super welter wa Afrika (ABU) kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Mei 28,2021.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa ( wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini mbalimbali mara baada ya kuzindua pambano la Rumble in Dar 2 ambapo bondia Hassan Mwakinyo atazichapa na Brendon Denes wa Zimbabwe Mei 28 kwenye ukumbi wa Next Door Arena.
Meneja Masoko wa M-Bet Tanzania, Allen Mushi akifafanua kuwa wameamua kuingia katika ngumi za kulipwa kwa lengo la kupanua wigo wa shughuli zao na kwamba M-Bet kwa sasa inadhamini timu ya Ligi Kuu ya KMC na wanajisikia fahari kubwa kudhamini ngumi za kulipwa kwani ni mchezo namba mbili hapa nchini.
Mkuu wa Masoko wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo akifafanuza jambo kwa Waandishi wa habari,kwamba pambano la #RUMBLEINDAR linatarajia kuonekana katika nchi zaidi ya 32 za Afrika na nchi mbalimbali duniani kupitia DStv app.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Jackson Group Sports, Kelvin Twissa,Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki ya KCB Christine Manyenye,Mkuu wa Masoko wa kampuni ya Multichoice Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzungumza na vyombo vya habari mkoani Dar es Salaam.
No comments: