KWA SASA TANZANIA IMEWEZA KUDHITI VIZURI CORONA NA WANANCHI WAENDELEE KUTEKELEZA MBINU ZOTE ZA KINGA .

Na.WAMJW-Mwanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi amewaondoa hofu Watanzania,wageni pamoja na watalii juu ya ugonjwa wa corona(COVID-19)  kwa sababu Serikali na Wananchi wameendelea kuudhibiti vizuri mpaka sasa.

Prof.Makubi ameyasema hayo wakati alipo tembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou -Toure  ambapo alipata fursa ya kukagua idara mbalimbali  ikiwemo chumba cha CT-Scan pamoja na kuzungumza na wagonjwa walikuwa wakipata matibabu katika hospitali hiyo.

Wasafiri pamoja na watalii waendelee kuja nchini bila wasiwasi lakini kuna utaratibu wanapewa huku Watanzania wakiendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga ili udhibiti uliopo sasa uendele zaidi na ndio suala la msingi ambalo anawaomba  wananchi waendelee kukaza na wasilegeze kamba katika kutii maelekezo ya kuchukua tahadhari zote dhidi ya corona.

Amesema Serikali imeendelea kudhibiti tatizo la COVID-19 mpaka sasa  hivyo amewathiibitishia wananchi kuwa taifa lipo katika hali nzuri  ya udhibiti wa ugonjwa huu.

Pia amesema Rais Samia Suluhu Hassan,ameweka mfumo mzuri wa kushughulikia suala hili na mpaka sasa hivi wanaweza kuona udhibiti zaidi kutoka kwa Wananchi.

"Sisi kama Wizara tunaona tupo kwenye hali nzuri,sasa hivi tumeidhibiti sana COVID-19 pengine kuliko nchi yoyote ile,na jitihada hizi zilianza kuanzia mwaka jana kwenye Serikali ya awamu ya tano na zimepokelewa na kuendelezwa vizuri na Serikali hii ya awamu ya sita," amesema Prof.Makubi.

Hata hivyo amesema,kinachopaswa kufanywa na wananchi kwa sasa ni kuhakikisha wanatii na kuyafuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu kwani amepita katika hospitali hiyo ya Sekou- Tou're amekuta miundombinu mizuri imewekwa ya kujikinga na COVID-19 ikiwemo sehemu za kunawia mikono na watoa huduma wanavaa barakoa kwani ni eneo ambalo lina hatari kubwa hivyo lazima wajikinge na kuchukua tahadhari zote.

"Niwaambie Watanzania wote na wasafiri muendelee kuwa na amani na  wananchi  muendelee kuchukua tahadhari kwani awali mmeweza kuchukua tahadhari vizuri sana na ndio maana tumeweza kudhibiti ,niendelee kuwapongeza Watanzania kwa sababu haya ni matunda ya wao kuwa wasikuvu,"amesema Prof.Makubi.

Aidha, Prof. Makubi amesema,tofauti na kunawa mikono na kuvaa barakoa  pia kuna njia nyingine ya kujikinga na COVID-19 ambazo ni pamoja na kupunguza misongamano isiyokuwa ya lazima.

Pia kufanya mazoezi kwani ugonjwa huu unaathiri sana watu ambao wanamagonjwa ambayo siyo ya kuambukiza kama kisukari,shinikizo la damu na moyo.

Pamoja na kuzingatia lishe bora ambayo inasaidia kinga za mwili kama matunda pia kumekuwa na tiba za asili ambazo nazo zinapaswa kuendelea kuhamasishwa na wakiendelea kuzingatia hayo yote ugonjwa huo wataendelea kuudhibiti na pengine kuudhibiti zaidi hivyo hakuna haja ya watu kuwa na hofu.

"Tunapo fanya mazoezi inasaidia,tumeona wana michezo wengi wameweza kupata ugonjwa huu katika nchi zilizoendelea lakini sijasikia kifo, wengi wameweza kuudhibiti kwa kutumia kinga  ya mwili wao  na baadae ugonjwa unaisha,hivyo mazoezi tuendelee kuyafanya  angalau mara tatu au nne kwa wiki angakau nusu saa hadi mwili utoe jasho pia tuzingatie lishe,"amesema Prof.Makubi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi(kulia) akiwa na Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa( kushoto) wakati alipo tembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou -Toure  ambapo alipata fursa ya kukagua idara mbalimbali  ikiwemo chumba cha CT-Scan pamoja na kuzungumza na wagonjwa walikuwa wakipata matibabu katika hospitali hiyo.picha na Judith Ferdinand






 

No comments: