KISARAWE YAZINDUA KAMPENI YA KUTOKOMEZA KICHAA CHA MBWA NA PAKA TANZANIA
*Asilimia 25 ya mbwa milioni 4.5 nchini na paka laki tano wachanjwa
IKIWA imepita miaka mitano tangu Tanzania iweka kipaumbele kwa magonjwa kadhaa ambukizi ikiwemo kichaa cha mbwa yanayotakiwa kutokomezwa kabla ya 2030, mtandao wa afya wa vyuo vikuu Afrika "The Africa One Health University Network (AFROHUN,) umezindua kampeni hiyo katika Wilaya ya Kisarawe kwa kuchanja mbwa na paka ili kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amesema, kampeni hiyo ya uchanjaji wa mbwa na paka ni muhimu kwa kuwa tatizo hilo limekuwa kwa muda mrefu ambapo watu hung'atwa na kupoteza maisha kwa kuwa ugonjwa huo hauna matibabu hadi sasa.
Amesema, kampeni hiyo iliyozinduliwa Mkoani Morogoro ilijadili kwa undani kuhusu suala la kichaa cha mbwa na paka na kukubaliana kufanya kampeni ya kuchanja mbwa na paka wote wilayani Kisarawe kwa kutumia nguvu kazi ya wanafunzi wa vyuo vikuu.
"Kazi hii imepangwa kufanyika kwa ushirikiano baina ya wanafunzi wa afya ya binadamu kutoka MUHAS na wale wa afya ya wanyama kutoka SUA ambao wana ujuzi mkubwa wa kuchanja aina zote za wanyama, kuelimisha jamii juu ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa na namna ya kuutokomeza, pia wanafunzi hao watakuwa na jukumu la kuhamasisha jamii katika kampeni hii inayokwenda sambamba na kauli mbiu ya "Linda Afya Yako na ya Jamii Kwa Kuwachanja Mbwa na Paka Wako." Amesema Mwegelo.
Pia amesema kampeni hiyo ni endelevu na wataendelea na utaratibu wa kushirikiana na Wanafunzi hao kila mwaka kama nguzo muhimu ya kuhudumia jamii, kudhibiti pamoja na kutokomeza magonjwa yanayowakabili wanajamii na tayari vyuo vikuu, TAMISEMI na Wizara husika wameshaombwa kushiriki utaratibu huo ili kuleta matokeo chanja.
Vilevile ameupongeza mtandao wa AFROHUN, Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhuisha dhana ya afya nchini na kufanikiwa kujenga kikosi kazi cha wataalamu wa afya kwa wanafunzi waliopo vyuoni na watumishi.
Mwegelo amewashukuru AFROHUN, MUHAS, SUA, Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO,) Umoja wa Kimataifa, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Taasisi ya Afya ya Ifakara kwa mchango wa kufanikisha kampeni hiyo pamoja na USAID kupitia chuo kikuu cha UC DAVIS, Marekani kwa kutoa fedha za kuendesha shughuli hiyo na nyingine nyingi nchini Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Hezron Nonga ameishukuru AFROHUN kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo imewahusisha wanafunzi wanaotegemea kuhitimu masomo yao ambao wameongeza nguvu kazi katika utoaji wa chanjo.
Aidha amewataka wamiliki wa mbwa na paka kote nchini kujitokeza kuchanja mifugo hiyo ili kuepukana na maradhi ya kichaa cha mbwa.
"Tafiti zinaonesha kuna mbwa milioni 4.5 na paka zaidi ya milioni mbili nchi nzima na Wilaya ya Kisarawe pekee ina mbwa na paka wapatao 4602 hivyo lazima wamiliki wa wanyama hao wajitokeze kuwachanja ili kuwalinda na kumlinda binadamu ambaye ndiye muathirika wa mwisho." Amesema.
Pia amesema kuwa zaidi ya watu 3387 hupata majeraha ya kuumwa na mbwa yasiyoleta madhara ya kichaa huku matibabu yake yakigharimu zaidi ya laki mbili huku chanjo kwa wanyama hao ikiwa ni kati ya shilingi 2000 na 3000.
Amesema katika mkakati wa kidunia wa kukomesha kichaa cha mbwa ifikapo 2030 chanjo kwa wanyama hao ni lazima na hadi Aprili 30 asilimia 25 ya mbwa na paka laki tano walipata chanjo hiyo.
Ameeleza kuwa ndani ya wiki moja watatoa elimu kwa wananchi wa Kisarawe juu ya umuhimu wa kuchanja mbwa, madhara ya kichaa cha mbwa na ufugaji kwa ujumla.
Kwa upande wake Meneja wa Mtandao wa AFROHUN Tanzania, Prof. Japhet Killewo amesema katika kampeni hiyo watashirikiana na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya MUHAS na SUA na kuwahimiza wananchi wa Wilaya hiyo kuchanja mbwa na paka kwa kuwa Kisarawe ni Moja ya Wilaya inayoongoza kwa tatizo hilo kutokana na ukaribu wake na mbuga ya 'Selous Game Reserve.'
Killewo amesema, katika kampeni hiyo wanafunzi wa wanyama kutoka SUA wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuchanja mbwa na wanafunzi wa afya ya binadamu kutoka MUHAS watashiriki katika kusajili mbwa na wamiliki, kuelimisha wamiliki wa wanyama hao juu ya umuhimu wa chanjo hiyo, dalili na madhara ya kichaa cha mbwa, kutoa taarifa za uchanjaji pamoja na kutoa vyeti vya chanjo.
Ameeleza kuwa wanafunzi hao watapata fursa ya kukutana na wataalamu wabobezi wa afya na kupata maarifa mapya na kila mwaka wanafunzi watachaguliwa kushiriki katika mafunzo ya namna hiyo.
Tafiti zinaeleza kuwa watu 70,000 duniani hufariki kutokana na kichaa cha mbwa na kwa Tanzania watu 1,500 hupoteza maisha kutokana na kichaa cha mbwa huku juhudi mbalimbali zikiwekwa katika kutokomeza tatizo hilo ikiwemo kutoa chanjo kwa wanyama hao.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo wa pilia kushoto akishuhudia Mbwa akichomwa sindano ya chanjo kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa Kichaa cha Mbwa kutoka kwa Wataalamu wa Wanyama chuo SUA na MUHAS,wakati wa kuzindua kampeni maalum ya Kitaifa ya kuzuia Kichaa cha Mbwa na Paka, itakayoendelea kutolewa kwa Wanyama hao katika Kata zote za wilaya ya Kisarawe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo wa pili kushoto akimkabidhi mmiliki wa Mbwa kadi ya chanjo mara baada ya kuchomwa mbwa huyo,ikiwa ni sehemu ya kuzindua kampeni maalum ya Kitaifa ya Mbwa na Paka itakayoanza kutolewa kwa Wanyama hao katika Kata zote za wilaya ya Kisarawe
Mmoja wa Wataalamu masuala ya Wanyama kutoka SUA akimchima paka sindano ya chanjo kwa ajili ya kuzuai magonjwa mbalimbali hatarishi kwa Wanyama ,ikiwa ni sehemu ya kuzindua kampeni maalum ya Kitaifa ya Kichaa cha Mbwa na Paka itakayoendelea kutolewa kwa Wanyama hao katika Kata zote za wilaya ya Kisarawe.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo akipokea vifaa mbalimbali kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Shirka la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Tanzania,Prof.Folorunso Fasina (kulia),Vifaa vitakavyotumika katika shughuli ya Chanjo ya Kichaa cha Mbwa na Paka wilayani huyo.
No comments: