Dk. Chamuriho awapa neno makandarasi wazalendo kuhusu rushwa

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho katikati akiwa ameshika hundi yenye thamani ya Sh milioni 5 iliyotolewa na Kampuni ya Derm Electrics Limited kusaidia kufanyika kwa mkutano wa mashauriano ya makandarasi wazalendo ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB).
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho (katikati) akizungumza na Mjumbe wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Steven Makigo kulia na Mwenyekiti wa (CRB), Injinia Consolata Ngimbwa wakati alipowasili  kwaajili ya kufungua mkutano wa mashauriano baina ya wadau wa sekta ya ujenzi iulioandaliwa na CRB jana Mkoani Dar es Salaam.

*Aipongeza bodi ya CRB kwa kuwapa mafunzo makandarasi

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka makandarasi kuwafichua maofisa wa serikali wanaowaomba rushwa ili wawape upendeleo kwenye zabuni za ujenzi ili hatua kali ziweze kuchukuliwa dhidi yao huku ikisifu juhudi zinazofanywa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo ili waweze kutekeleza miradi mikubwa.

Hayo yamesemwa leo Mei 27, 2021 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa mashauriano wa wadau wa sekta ya ujenzi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

Amesema mkandarasi anapopewa mradi kwa kutoa rushwa mara nyingi miradi haikamiliki kwa wakati na wakati mwingine inafanywa kwa viwango vya chini hivyo kuisababishia serikali hasara kubwa kwa kuharibika kwa muda mfupi.

“Sekta ya ujenzi ni eneo ambalo linalalamikiwa sana kwa rushwa hivyo ungeni mkono juhudi za serikali katika kupambana na vitendo vya rushwa kwasababu kupata zabuni kwa rushwa hakukuendelezi bali kunakudidimiza.” alisema Waziri Chamuriho

Vile vile, Waziri amesema huu ni wakati mwafaka kwa makandarasi wazalendo kuungana na kutumia fursa zilizopo kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi kwa kuweka ubinafsi pembeni.

Amesema kazi nyingi za ujenzi zinafanywa na makampuni ya nje kutokana na makandarasi wa ndani kukosa uwezo wa mitaji, mitambo ya kutosha na rasilimali watu hivyo kuungana ndiyo itakuwa suluhisho la matatizo yao.

“Serikali haifurahii kuona kandarasi kubwa kubwa zinafanywa na makampuni ya nje, acheni ubinafsi muungane mpate uwezo wa kuzifanya nyinyi kwasababu mkizifanya nyinyi gharama zitashuka na fedha zitabaki nchini.” Amesisisitiza

Waziri Chamuriho pia ameahidi kutoa tamko kuhusu utaratibu unaotumiwa na serikali kufanyakazi za ujenzi bila kutumia makandarasi maarufu kama Force Account, ambao umelalamikiwa na makandarasi.

Amesema serikali itatoa tamko hilo mwezi Juni kwenye mkutano wa mashauriano baina ya Bodi yaUsajili wa Makandarasi (CRB) na wadau wa sekta ya ujenzi unaotarajiwa kufanyika mkoani Mwanza mwezi Juni.

“Serikali inalifanyia kazi hilo na hata Mwenyekiti wa Bodi ya CRB amelizungumza hapa muwe wavumilivu tutalitolea tamko mwezi Juni mwaka huu kwenye mkutano wanne utakaofanyika mkoani Mwanza.” Alisema Waziri Chamuriho.

Waziri ameyasema hayo baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi, Mhandisi Consolatha Ngimbwa kumweleza kuwa utaratibu huo umesababisha maumivu makubwa kwa makandarasi wa ndani kwani kwa muda mrefu hawana kazi.

Alimweleza Waziri kuwa mwaka 2018 serikali iliamua kutumia utaratibu huo ikisema kuwa makandarasi wa ndani wamekuwa wakitoza fedha nyingi ambazo haziendani na miradi husika hivyo kulazimika kutekeleza miradi yake yenyewe ili kukoa fedha nyingi.

Mhandisi Ngimbwa alisema makandarasi wameshajifunza na wako tayari kuanyakazi kwa bei ya chini na kwa ubora wa hali ya juu kwani wameshapewa mafunzo ya mara kwa mara na bodi ya CRB na kwa sasa wameiva kufanyakazi hizo.

“Baada ya serikali kuanza utaratibu wa force account kwa maelezo kuwa bei za makandarasi wa ndani ni kubwa tuliwapa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu namna ya kujaza zabuni, tulienda mikoa mbalimbali na kwa kweli wameiva na wako tayari kufanya kazi za serikali.” Alisema

No comments: