COSTECH YATAKIWA KUJENGA KITUO CHA UUNIFU BAGAMOYO
Mkurugenzi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Watu (HDIF), Joseph Manirakiza akizungumza wakati wa uzinduzi wa maonesho ya saba ya wiki ya Ubunifu yaliyoanza leo Mei 17, 2021 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa LAPF Kijitonyama, mkoani Dar es Salaam.
Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kapanga, akizungumza wakati akifungua Maonesho ya wiki ya ubunifu leo Mei 17, 2021 katika kumbi za LAPF Kijitonyama, Dar es Salaam
Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kapanga (wa katikati mbele) Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe ( kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Amos Nungu na wageni mbali mbali, wakifuatilia uzinduzi wa Maonesho ya wiki ya ubunifu leo Mei 17, 2021 katika kumbi za LAPF Kijitonyama, Dar es Salaam
Baadhi ya wafanyakazi wa HDIF wakifuatilia ufunguzi wa wiki ya ubunifu
SERIKALI imesema iko katika hatua ya mwisho ya kufanya mapitio ya sera ya sayansi na teknolojia ili kuendana na hali ya ubunifu wa kidigitali na kuzifanya kuwa bidhaa zinazouzika.
Sera hiyo itasaidia kuwaleta, kuwatambua wabunifu na kuwaendeleza ili waweze kuleta mabadiliko ya kidigitali.
Aidha serikali imeitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH ), kujenga kituo cha ubunifu katika kijiji cha Bagamoyo kitakachowakutanisha wabunifu na bunifu zao mbalimbal ili watu waweze kujifunza namna ya kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.
Kipanga amesema serikali itahakikisha inaendelea kuboresha mazingira ya biashara katika kuchangia ukuaji wa uchumi kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika teknolojia na pia kuratibu, kusimamia na kuzifanya bunifu zote kuwa bidhaa na kwamba ni wakati wa wabunifu hao kubuni vitu vyenye tija ili kutatua changamoto kwenye jamii.
Ameongeza kuwa, serikali pia itaendelea kuimarisha miundombinu yote ya mawasiliano kwani mawasiliano yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi, Lakini serikali pekee haitaweza kuleta mabadiliko ya hayo endapo hatutashirikisha wadau, wabunifu na wafadhili.
"Ubunifu umechangia katika kuongeza ajira kwani huduma nyingi zinatolewa kwa njia ya mtandao ikiweko ulipaji wa bili mbalimbali ikiwemo maji, umeme na leseni za biashara na hata kutuma pesa kwenda umbali wowote.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa HDIF Joseph Manirakiza amesema, mpango wa Maendeleo wa miaka mitano umeelezea umuhimu wa kukuza ubunifu na teknolojia katika kuongeza uzalishaji na kutoa nafasi katika kuchangia ukuaji wa uchumi kidigitali.
Amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo miaka saba iliyopita HDIF imechangia ukuaji wa masuala ya ubunifu nchini ambapo mpaka sasa imeishafadhili miradi 48 kutoka kwa wabunifu wadogo 55 na atimizi kupitia mashindano kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
"Tunajivunia mafanikio makubwa ya kuibua wabunifu na kuifanya wiki hii kuwa kubwa ambapo sasa serikali kupitia Waziri Mkuu ametutaka wiki ya ubunifu iwe inafanyika kila mwaka kuanzia ngazi ya Mkoa Wilaya hadi taifa na mwaka huu mbali na Dar es Salaam mikoa mingine yanakofanyika maonyesho hayo ni, Arusha, Zanzibar, Morogoro, Iringa, Mbeya, Mwanza na Tanga.
Hivi karibuni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu alisema dunia ipo katika Mapinduzi ya nne ya viwanda na kwamba uchumi wake unategemea teknolojia, Tanzania haiwezi kubaki nyuma katika kuwekeza katika sekta hiyo ya kidigitali kama utakumbuka wakati wa corona shule chache ndizo zilikuwa zinaendelea kutoa elimu wakati shule zilipofungwa na ni kwa sababu waliwekeza katika teknolojia hiyo ya kisasa iliyoibuliwa na ubunifu.
"Tumefanya kazi pamoja na serikali kupitia Costech na wakati mwingine wizara lengo likiwa kubadilishana uzoefu na uelewa. Tumewasaidia Costech katika kuwasaidia wabunifu na watafiti lakini ubunifu Tanzania bado unahitaji fedha, kuwajengea wabunifu uelewa na kuweka mazingira wezeshi kwa kuboresha sera".
Alisema wamekuwa wakitoa fedha na masuala ya kiufundi katika bunifu zinazogusa sekta za maji, afya na elimu na kuchangia kuimarisha ubunifu katika kutatua changamoto katika jamii.
Aidha Manirakiza amewataka wabunifu kuhakikisha wanaendelea kubuni vitu vyenye kutatua changamoto kwa jamii na kwa upande wa serikali kuendeleza mfumo huo katika kuongeza uzalishaji, kufanya mapitio ya sera ili kukuza teknolojia na wafadhili waendelee kushirikiana na serikali kuhakikisha ubunifu unakua nchini.
Wiki hiyo ya Ubunifu nchini imeandaliwa na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Binadamu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).
No comments: