GAVANA LUOGA AIPONGEZA STAMICO KUANZA KUCHAKATA DHAHABU

 

Benki Kuu ya Tanzania imelipongesha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa hatua iliyofikia ya kuanza usafishaji wa dhahabu hapa nchini kwa ubora wa kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, wakati alipotembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Minerals Limited, kilichopo jijini Mwanza Ijumaa na kujionea maendeleo yaliyofikiwa hadi sasa, ikiwemo kuanza uzalishaji.

“Haya ni mapinduzi makubwa katika sekta ya madini na ukombozi kwa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta hii. Ndoto ya Tanzania kuacha kusafirisha dhahabu ghafi naona inaelekea kutimia”, alisema Gavana Luoga.

Aidha, Prof. Luoga alivutiwa na taarifa kwamba kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa kwa ubia kati ya serikali kupitia STAMICO na wawekezaji wa nje, pia kina uwezo wa kutenganisha dhahabu na madini mengine ambayo yana thamani katika masoko ya madini duniani.

“Kwa uwezo wa kiwanda hiki, nina imani mtaweza kununua dhahabu yote nchini na nchi jirani na kwa kuwa dhahabu inayotoka kiwandani hapa itakuwa na nembo ya Tanzania, itaitangaza nchi kimataifa” alisema Gavana wa Benki Kuu.

Katika kiwanda hicho, STAMICO inamiliki asilimia 25 wakati asilimia zilizobaki 75 zinamilikiwa kwa pamoja na kampuni za ROZZELA General LLC ya Dubai, Umoja wa Walme za Kiarabu (UAE) na ACME Consultant Engineers PTE Limited ya Singapore (RGTACE).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, alimweleza Gavana Luoga kuwa “katika ubia huu, hisa za STAMICO zitakuwa zinaongezeka kwa asilimia tano (5), ambapo baada ya miaka 15 STAMICO itakuwa imefikisha asilimia 51 na wabia wengine kubaki na asilimia 49.

Alieleza pia kwamba katika ubia huo, STAMICO itakuwa inapata asilimia 2.5 ya mauzo ghafi kwa huduma za usimamizi (Management fee) zinazotolewa na Kampuni”.

Kiwanda hicho kimeanza uzalishaliji wa majaribio tarehe 21 Aprili 2021. Kina uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu kwa siku kwa ubora wa kimataifa (999.9 purity) ni kitakuwa kimojawapo cha viwanda vikubwa vya kusafisha dhahabu barani Afrika.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO alieleza kuwa faida za uwekezaji huo ni nyingi zikiwemo kuchangia mapato ya nchi kupitia ada za ukaguzi, kuongeza mapato ya halmashauri kupitia tozo mbalimbali, ajira, teknolojia ya kisasa ya kuchakata dhahabu na kupunguza utoroshaji wa dhahabu inayochimbwa Tanzania.

Aidha, kupitia kiwanda hicho, dhahabu ya Tanzania itatambulika kupitia nembo yake maalum ya uasili (originality mark), madini mengine yataweza kuainishwa na kuthaminishwa hapa nchini na kuiwezesha Benki Kuu kuanza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria za nchi.

Gavana Luoga ambaye aliambatana na wataalam mbalimbali wa Benki Kuu, aliwaeleza umuhimu wa kuwa na hati ya utambuzi ya kimataifa (accreditation) ili kuiwezesha Benki Kuu kununua dhahabu hiyo kama sehemu ya akiba ya fedha za kigeni za nchi (foreign reserves).

Kiwanda hiki kimejengwa kimkakati kikiwa katikati ya mikoa izalishayo dhahabu kwa wingi kama Geita, Mara, Shinyanga na Mwanza yenyewe. Kiwanda kinategemea kitakua kinapata dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wachimbaji wakubwa wenye migodi hapa nchini, dhahabu zilizotaifishwa na serikali, dhahabu kutoka nchi jirani na dhahabu kutoka kwa madalali (dealers).

Uwekezaji huo, siyo tu utaongeza mapato yatokanayo na madini, bali pia utaipa heshima nchi ya Tanzania kwa kuwa usafishaji wa dhahabu utakuwa wa viwango vya kimataifa.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga, akiangalia dhahabu iliyosafishwa kufikia kiwango cha 999.9 (purity) wakati alipotembelea kiwanda cha Mwanza Precious Minerals Limited. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Bw. Venance Mwasse.

No comments: