MILIONI 700 ZAMALIZA KERO YA MAJI KIPAPA NA MHILO


Na Muhidin Amri, Mbinga
MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa),imekamilisha ujenzi wa miradi miwili ya maji kwa mafanikio makubwa katika vijiji vya Mhilo na Kipapa katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Kukamilika kwa miradi hiyo kumemaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji hivyo ambao kabla ya ujenzi wa miradi hiyo, walilazimika kutumia maji ya visima vya asili vilivyochimbwa kienyeji na wengine kwenda mtoni kuchota maji ambayo hayakuwa safi na salama.

Meneja ufundi wa Souwasa Jafari Yahaya alisema, Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 772 ili kujenga miradi yote mwili iliyohusisha ujenzi wa matenki, miundombinu mbalimbali na vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa katika makazi ya watu na kwenye taasisi za umma.

Akizungumzia mradi wa Kipapa Jafari alisema, serikali kupitia wizara ya maji imetoa shilingi milioni 569 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na kuboresha huduma ya maji ambapo kati ya hizo, tayari imetoa milioni 444 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Alisema, kazi zilizopangwa na zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo,ujenzi wa tenki la kusambazaji maji,usambazaji wa bomba za kusafirishia na kusambaza maji na kujenga vituo 23 vya kuchotea maji.

Kwa mujibu wake,kazi zimekamilika kwa asilimia 98 na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama, isipokuwa ujenzi wa uzio ambao hajakamilika na unaendelea kujengwa.

Aidha katika mradi wa Muhilo Jafari alisema, Serikali imetoa shilingi milioni 203 na kazi zilizofanyika ni ujenzi wa tenki wa lita 50,000 na shughuli nyingine ambapo wakazi 1,247 wamenufaika na mradi huo.

Aliongeza kuwa, serikali imetoa fedha hizo kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa wananchi wa maeneo hayo ili watumie muda mwingi kufanya shughuli za maendeleo, badala ya kupoteza muda wao kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.

Alisema, miradi yote ipo chini ya wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) mkoa wa Ruvuma na Souwasa ilipewa kazi ya kujenga kama fundi.

Jafari alisema, miradi yote imekamilika kwa asilimia 98 na sasa wananchi wanapata huduma ya maji katika maeneo yao pamoja na taasisi za serikali kama shule na zahanati na kuishukuru Ruwasa kwa kwa kuwaamini na kuwapa kazi ya Ujenzi wa miradi hiyo.

Manfred Nchimbi(56) mkazi wa Kipapa alisema, awali walilazimika kuamka saa 9 usiku na kutembea umbali wa km 3 kwenda kutafuta maji, lakini sasa kero hiyo imemalizika na kuishukuru serikali kupitia wizara ya maji kutekeleza mradi huo ambao umemaliza kabisa mateso ya muda mrefu.

Alisema, kabla ya kujengwa kwa mradi huo na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) chini ya fundi Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Songea(Souwasa) walitumia maji kutoka katika vyanzo visivyo rasmi lakini havikutosheleza mahitaji yao.

Kanisia Komba mkazi wa kijiji cha Mhilo,mbali na kuishukuru serikali kwa kupeleka huduma ya maji katika kijiji hicho alisema, maji hayo yamerudisha na kuboresha mahusiano na kuimarika ndoa zao.

Alisema, baadhi ya ndoa zimevunjika kwa sababu ya akina mama kuchelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji, hivyo wanaume kudhani walikuwa kwenye michepuko(nyumba ndogo) jambo ambalo lilichangia ndoa nyingi kuvunjika na kusambaratika kwa familia.

No comments: