KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE NSSF YATOA MSAADA WA VIFAA TIBA HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Wafanyakazi wa NSSF na watumishi kutoka hospitalini ya Rufaa Mwananyamala wakiwa wameshika moja ya shuka mara baada ya makabidhiano, leo Mkoani Dar es Salaam. Wafanyakazi wa NSSF na watumishi kutoka hospitalini ya Rufaa Mwananyamala wakiwa wameshika makasha ya mipira 'Gloves' mara baada ya makabidhiano, leo Mkoani Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa NSSF wakiwa wameshika mashuka waliyokabidhi katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa matumizi ya wodi ya wazazi, leo Mkoani Dar es Salaam.
*****************************
Na Amiri Atick, Michuzi Tv
KATIKA Kuadhimisha siku ya wanawake duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 8, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF,) limetoa msaada wa vifaa kwa wodi ya wazazi katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Mkoani Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuokoa maisha ya wanawake wajawazito na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo hospitalini hapo Meneja uhusiano na Elimu kwa Umma kutoka NSSF, Lulu Mengele amesema, katika kuadhimisha siku ya mwanamke ulimwenguni Shirika hilo limekuwa likiwashika wanawake mkono kwa namna mbalimbali ili kuonesha thamani na umuhimu wao katika jamii.
Lulu amesema, walifika hospitalini hapo na kuona uhitaji wa mipira (Gloves,) na mashuka na kwa kuona umuhimu wa suala hilo wakaona washiriki kwa kuchangia vifaa hivyo ambavyo ni mashuka na mipira (Gloves,) inayotumika wakati wa kujifungua na vyote kwa pamoja vimegharimu shilingi milioni nane na laki saba.
Aidha amesema, hivyo vilivyotolewa hospitalini hapo vitawasaidia wajawazito kujifungua wakiwa na uhakika na usalama wao.
"Wadau wengine wakijitokeza tutaweza kutatua changamoto hii na kuwaweka wajawazito uhakika wa usalama wao pamoja na watoto wao." Amesema.
Lulu, amewashauri wanawake kutumia fao la uzazi la NSSF linalotolewa kwa wanawake pindi wanapojifungua ili waweze kulea watoto wao kwa usalama zaidi.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Dk. Daniel Mkungu amewashukuru NSSF kwa msaada huo ambao utasaidia wodi ya wazazi hospitalini hapo.
Makungu ametaka wadau wengine kufuata nyayo zinazofanywa na NSSF katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo katika sekta ya afya.
Mmoja wa wanufaika wa msaada huo Rose Robert amewashukuru NSSF kwa kuwawekea mazingira bora zaidi katika wodi wazazi na kueleza kuwa mazingira bora huleta uhakika na usalama wa uzazi wao kabla na baada ya kujifungua.
No comments: