BI.TELACK AWATAKA WANAWAKE KUZINGATIA MAADILI KUPUNGUZA ULAWITI NA UBAKAJI
Na Mwandishi wetu- Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack amewataka wanawake nchini kuzingatia suala la maadili katika malezi ya watoto ili kuweza kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti kwa wanawake na watoto Nchini.
Bi. Telack alisema hayo jana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani Mkoani Shinyanga yaliyoadhimishwa kimkoa katika Kata ya Ulowa iliyoko katika Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuwakutanishwa makundi tofauti ya wanawake mkoani humo kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.
‘’Wanawake tunaweza kutokomeza ubakaji na ulawiti kwa watoto kama tutaweza kufahamu ni wapi aliko mtoto wako kila wakati, rafiki zake ni akina nani, na nacheza na akina nani na hili litapunguza ukatili dhidi ya watoto’’. Alisema Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack.
Bi. Telack amewataka wanawake kote nchini kudhamilia kwa pamoja kutokomeza ukatili dhidi ya watoto kwani uwezo wa kutokomeza ukatili wanao kama watazingatia zaidi kutoa malezi kwa watoto kwa kuzingatia maadili katika jamii.
Aidha Bi. Telack amewataka akina mama kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili waweze kutoa mchango mkubwa wa kiuchumi katika familia zao na kwa taifa lakini pia wasaidiane na waume zao kuinua hali ya kipato cha familia kwa kufanya kazi bila kukata tamaa kwakuwa hali ya maisha imebadilika na sio kuwaachia wanaume peke yao.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Albert Msovela amesema tafiti zilizopo zinaonesha bado kuna vitendo vya ukataili katika jamii na mmomonyoko wa maadili kwa watoto unaochangiwa na wazazi na walezi kutokuwa karibu na watoto wao.
Bw. Msovela aliongeza kuwa mkoa wa shinyanga umedhamilia kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, watoto na mabinti kwa kuwawezesha wanawake lakini pia kutoa elimu ya masuala ya ukatili kwa kupitia vikundi mbali mbali vilivyopo hususani vile vya kiuchumi.
Maadhimisho haya yamefanyika katika ngazi ya Mkoa kote Nchini na yanalenga kutoa ujumbe kwa jamii kuwa nafasi ya mwanamke katika nafasi mbalimbali za uongozi ni chachu ya kufikia dunia yenye usawa kama kauli mbiu ya maadhimisho haya inavyosema, kuwa wanawake katika uongozi chachu kufikia dunia yenye usawa.
Serikali Mkoani Shinyanga imeungana na mikoa mingine nchini kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ambayo uadhimishwa Kimataifa kila ifika Machi 8, kila mwaka maadhimisho ambayo yamefanyika katika ngazi ya mkoa katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akicheza musiki na baadhi ya watumishi wa umma waliofika katika viwanja vya shule ya Msingi Kangeme Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu Kahama Shinyanga jana. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Jasinta Mboneko.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack akicheza musiki na baadhi ya wanawake waliofika katika viwanja vya shule ya Msingi Kangeme Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu Kahama Shinyanga jana.
Baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakifuatilia jambo kwa makini wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Kangeme Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu Kahama Shinyanga jana. Baadhi ya watumishi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga wakijumuika kwa pamoja kuadhimisha ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Kangeme Kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu Kahama Shinyanga jana.
No comments: