VIONGOZI WATOA YA MOYONI KUHUSU MHANDISI KIJAZI...ALIKUWA DARAJA

Na Said Mwishehe, Michuzi TV .


VIONGOZI mbalimbali nchini wametoa ya moyoni wakati wakitoa salamu zao kwenye shughuli za kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi John Kijazi.

Mhandisi Kijazi ameagwa leo katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo Rais Dk.John Magufuli ameongoza waombolezaji wakati wa shughuli hiyo.

Wakizungumza wakati wakitoa salamu hizo, viongozi mbalimbali wamuelekezea Mhandisi kama kiongozi aliyekuwa daraja kati yao na Rais na alisimama imara katika kutekeleza majukumu yake.

Akitoa salamu za Serikali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema leo ni siku ngumu kwa Watanzania ana kwa niaba ya watumishi wa umma ametoa pole kwa Mkuu wa Nchi Rais Dk.Magufuli kwa kuondokewa na Mtendaji aliyekuwa akifanya kazi yake kwenye Serikali yake.

"Ni kiongozi aliyesimamiaa miongozo, kanuni, taratibu na itifika za Serikali na leo hii tunamuaga kuelekea nyumba yake ya milele, ni jambo gumu kulipokea lakini hatua budu kukubali maana Mungu ndio mwenye kupanga.Tunatoa pole kwa familia ya marehemu, mke, watoto na ndugu wa marehemu. 

"Kaka mkubwa wa marehemu tumemsikindikiza pale Korogwe mwezi mmoja uliopita, sisi watumishi wakati tunamsikindikiza kaka mkubwa tulikuja kuwapa pole na kwa bahati mbaya leo tunakuja kumsindikiza yeye.

"Huyu kiongozi ambaye amelala leo mbele yetu amefanya kazi kubwa sana katika Serikali, amefanya kazi yake vizuri na alikuwa daraja, binafsi natambua, namfahamu, ndio alikuwa Meneja wa kwanza wa Tanroads Mkoa wa Lindi, amekuwa  Balozi , amewakilisha nchi yetu katika nchi rafiki.

"Alikuwa Katibu wa Baraza la mawaziri, tumepoteza kiongozi, na Rais tunapokupa pole tunajua ukaribu wako sio tu ukiwa Rais bali hata ulipokuwa Waziri wa Ujenzi, hivyo hili ni pigo kubwa kwako na familia, lakini tunachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kumuombea,"amesema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma ametoa salamu za muhimili wa Mahakama ya Tanzania nchini na kwamba wanaungana na watanzania wengine kutoa pole kwa Serikali na Rais Dk.Magufuli kutokana na kuondokewa na Mhandisi Kijazi.

Aidha amesema ni vigumu sana kwake kumuelezea Mhandisi Kijazi aliyoyafanya na kwamba ukiangalia ile picha utaona kuna mwaka ambao amezaliwa na kuna kitone ambacho kimeficha mambo mengi.

"Alikuwa ndio mtu wa kutupokea pale Ikulu na kwenye mpangilio wa viti mimi nilikuwa nakaa naye.Kuna sifa tatu za uongozi, na kwa muda ambao nimekuwa naye karibu ameonesha, na utumishi huo sio kwenye umma tu bali hata kwenye Mahakama.

"Kiongozi ni kuonesha njia , kiongozi lazima uoneshe njia, sifa ya pili ni kutoa muelekeo, Mhandisi Kijazi alikuwa anaonesha muelekea na sifa ya tatu taaswira yake, ukiangalia picha yake ni Katibu Mkuu Kiongozi na alikuwa kweli Katibu Mkuu Kiongozi,"amesema Profesa Juma.

Akiendelea kumuelezea Mhandisi Kijazi, Profesa Juma amesema pia alikuwa makini sana hata kwenye mambo madogo."Nakumbuka siku moja wakati tunafanya mazoezi kwa ajili ya tukio la kuapishwa kwa Rais, alisimama makini na ilikuwa kama siku ya tukio lenyewe, alikuwa akiangalia kila kitu kama kiko sawa, umbali wa viti, watu wamekaaje.

"Nilimuuliza kwanini unaangalia mambo madogo madogo sana, akanijibu Mungu yupo kwenye maeneo yote na hata hayo yanayoonekana madogo madogo na wanaofanikiwa ni wale ambao hawadharau mambo madogo ambayo wengine wanadharau,"amesema Profesa Juma.

Ameongeza kuna mambo mengi ambayo Mahakama walikuwa wanafanya na mengine yanahitaji kumfikia Rais kwa haraka, hivyo Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa rahisi kumfikisha ujumbe wao na kisha kumfikia Rais.

"Hivyo aliiwezesha Mahakama ya Tanzania kumfikia Rais kwa haraka, hata hivyo tusihuzunike sana kama ambavyo viongozi wetu wa dini wamesema wakati wa Ibada. Kwa hiyo ninamuomba Mwenyezi Mungu tuwe na moyo wa ustahimilivu na kikubwa ni kumuombea dua,"amesema

Wakati huo huo Naibu Spika Dk.Tulia Ackson amesema kwa niaba ya Spika wa Bunge wanatoa kwa familia ya Mhandisi Kijazi na kwa Rais Dk.John Magufuli na watanzania wote kwa msiba mkubwa ambao umelipata taifa.

"Lakini ndugu zangu hata tukisimama hapa mbele tukazungumza mengi hayataondoa yale ambayo familia inasikia kwa sasa kutokana na kuondokewa na ndugu yetu, hivyo tunawaombea kwa Mungu ili mpate moyo wa uvumilivu.

"Katika Biblia kitabu cha Ayub mstari wa 14 unaeleza binadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake si nyingi, lakini Biblia hiyo hiyo inatutegemea tufanye yaliyomema.Mhandisi Kijazi alikuwa mtu mwema , alikuwa mnyenyekevu na hata sisi tuliokuwa tunakiangalia cheo chake amekitendea mema,"amesema Dk.Tulia.











 












 

No comments: