JESHI LA POLISI KUCHUNGUZA HOSPITALI YA AGA KHAN YA JIJINI DAR, LAUWA MAJAMBAZI

Kamanda wa Polisi, kanda maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa akizungumza jijini Dar es Salaam leo.

*Ni Uchunguzi  wa kutoza gharama kubwa za matibabu
Na Mwandishi wetu, Globu ya Jamii
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kufanya uchunguzi katika hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam kwa tuhuma dhidi ya kutoza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma hospitalini hapo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Kamanda wa Polisi, kanda maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa amesema kuwa jeshi la Polisi
limepokea malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya Hospitali ya Aga Khan ya Jijini Dar es Salaam kutoza gharama kubwa za matibabu kwa wagonjwa wa matatizo kifua (Pneumonia) ambayo hupelekea matatizo ya upumuaji.

Aidha wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali hiyo, pindi wanapofariki dunia kumekuwa na tabia ya kuzuia miili ya marehemu na kudai kiasi kikubwa cha fedha kinyume na maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam baada kupokea malalamiko hayo limefungua Jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSMZ/CID/PE/34/2021 dhidi ya malalamiko hayo.

Hata hivyo Mambosasa amesema kuwa uchunguzi utakapokamilika na kubaini tuhuma hizi hatua kali za kisheria zitachukuliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto dhidi ya Hospitali hiyo.

Katika tukio lingine, Polisi Kanda Maalum Dar es salaam ilifanikiwa kuwaua majambazi na kukamata silaha moja aina ya Shortgun yenye No.MO1562004 ikiwa na risasi mbili ndani ya kasha.

Ingali mapema Februari 17, 2021 jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam lilipokea taarifa fiche kuwa kuna majambazi wamepanga kuvamia duka la wakala wa Benki na mitandao ya simu huko maeneo ya kimara Stop over kwa kutumia pikipiki mbili, ndipo Polisi kupitia kikosi maalum cha kupambana na uhalifu waliwafuatilia majambazi hao wakiwa njiani ghafla wakagundua kuwa wanafuatiliwa na askari mara wakaanza kurusha risasi hovyo, Polisi walijibu mashambulizi na kufanikiwa kuwajeruhi majambazi wawili na wengine wawili kutokomea na pikipiki mbili kusikojulikana na baada ya upekuzi eneo la tukio ilipatikana silaha hiyo na maganda matano ya risasi ya silaha aina ya bastola waliokuwa wakiitumia kurushiana na askari. Majambazi hao ambao umri wao unakadiriwa kuwa kati ya miaka 30-40 walipelekwa Hospitali ya Mlonganzila na daktari aligundua kuwa wamefariki baada ya kuvuja damu nyingi.

Hata hivyo Katika tukio la tatu, kupatikana kwa silaha aina ya Bastola ya Mhe.Nape Nnauye (Mb) wa Mtama iliyoibiwa Februari 15, 2021 majira ya saa kumi na moja alfajiri huko nyumbani kwa maeneo ya Kawe Beach.

Bastola hiyo aina ya GLOCK 17 yenye No. YX647 ikiwa na risasi 14 ndani ya kasha lake. Silaha hiyo imekamatwa Feruari 17, 2021 mkoani Mbeya baada ya ushirikiano wa Jeshi la Polisi Kanda maalum Dar es Salaam na mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa mmoja anashikiliwa kwa tuhuma za wizi wa silaha hiyo.

No comments: