AGIZO LA MAGUFULI KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI WA BI ELIZABETH MANYONI LATEKELEZWA 100%
Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) akitoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kukabidhiwa hati ya eneo lake.
Na John Mapepele, Manyoni
MKUU wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ametekeleza agizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilomtaka kushirikiana na Viongozi wa Wilaya ya Manyoni kumrejeshea umiliki wa eneo lililokuwa mali ya Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) ambaye lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa kwa Kampuni mmoja ya simu za mikono ambayo imeweka mnara wa mawasiliano lirejeshwe mara moja kwa mama huyo ambaye ndiye ataingia mkataba wa upangaji na Kampuni hiyo.
Akikabidhi hati ya umiliki wa ardhi wa miaka 66 wa eneo hilo la Majengo Kiwanja Na 13 hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe, Dkt. John Pombe Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi wanyonge ili wapate haki zao na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo ili kuchangia katika uchumi wa kati na hatimaye uchumi wa juu wa Taifa letu.
Amesema Mkoa umejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi inakwisha mara moja kwenye Mkoa wa Singida na kuagiza Wakuu wote wa Wilaya na Wataalam wa ardhi kuanzia sasa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo husika badala ya kufanya mashauri ya migogoro ya ardhi maofisini.
“Kuanzia leo sitaki kuona shauri na migogoro ya ardhi ikitatuliwa maofisini, naagiza wakuu wote wa Wilaya katika Mkoa wangu na wataalam kwenda moja kwa moja kutatua migogoro ya ardhi ya wananchi katika maeneo ya migogoro, hatua kali zitachukuliwa kwa wote ambao hawatatekeleza agizo hilo” alisisitiza Mhe. Nchimbi
Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni amesema ni lazima iishe mara moja kwa kuwa Manyoni ya sasa ni Sebule ya Makao Makuu ya nchi-Dodoma na kwamba watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wanakuja Manyoni kwa kuwa kuna maeneo mazuri yenye fursa za uwekezaji hususan kwenye viwanda, biashara na kilimo cha zao la Korosho ambapo kwa sasa Wilaya hii inaongoza siyo tu Tanzania bali katika Bara la Afrika kwenye kilimo hicho ambapo kumekuwa na shamba la pamoja la Kilimo cha Korosho (Block Farming)lenye takribani ekari 25000.
“Haiwezekani Manyoni hii ambayo ni lango la makao makuu ya nchi ikaendelea kuwa na migogoro ya ardhi ambapo sasa ardhi yake imebeba uwekezaji mkubwa katika nchi yetu” aliongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa
Akipokea hati yake ya umiliki wa eneo hilo, Bibi Elizabeth Msalali alimshukuru Rais Magufuli kwa kusaidia kupatikana kwa kiwanja chake ambapo amesema Magufuli ameonyesha kuwa ni Rais anayewapigania watu masikini na wanyonge kama yeye hivyo anamwombea kwa Mungu azidi kumbariki katika utumishi na maisha yake kwa ujumla.
Aidha Mtoto wa pekee wa Bi Elizabeth ambaye ndiye aliyemwomba Mhe. Rais Magufuli kuingilia kati suala hili Bwana, Adamu Kazimoto alimshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuharakisha kukamilisha mchakato wa kupata hati ya umiliki wa kiwanja hicho kwa mama yake ambapo amesema mchakato huo umechukua muda mfupi sana.
“Naomba niwe mkweli kama tungekuwa na fedha ya kulipia hiki kiwanja nadhani ingechukua siku moja au mbili tu baada ya agizo la Mhe.Rais maana Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Dada Shamimu Hoza alikamilisha utengenezaji wa hati hiyo mara moja baada ya tamko hilo la Mhe.Magufuli jambo ambalo limetupa faraja kubwa kwani sasa mama yangu amepata haki yake” ameongeza Adamu
Akifafanua Adamu amesema suala hili alianza kufuatilia zaidi ya miaka tisa iliyopita, na anamshukuru Rais Magufuli kwa kutoa suluhisho la kudumu ambapo pia ameongeza kwamba mgogoro huo umeifanya familia ya Mzee Kazimoto kuwa kitu kimmoja licha sintofahamu ambazo zilikuwepo hapo awali kwa sababu ya tamaa ya pesa kwa wanafamilia.
Mhe. Rais John Pombe Magufuli alilitoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kushughulikia mgogoro huo tarehe 31Januari 2021 aliposimama kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini akitokea Tabora kwenda Dodoma.
Rais Magufuli alisikiliza kero inayowakabili wananchi hao ambao walilalamikia kitendo cha Idara ya Ardhi kuchukua maeneo yao bila kuwalipa fidia na wengine kuamriwa kuondoka katika eneo hilo baada ya kupewa nyaraka za kupatiwa radhi(offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo hilo na Idara ya Ardhi.
Rais ameagiza wananchi wenye offer waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa na wamiliki wa asili wa eneo hilo kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria.
Awali, kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais, Timu Maalum ya wataalam kutoka Mkoani na Wilaya ya Manyoni iliyoongozwa na Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Shamimu Hoza Shaban ilikutana familia nzima ya mmiliki wa asili wa eneo hilo marehemu Salum Kazimoto aliyefariki mwaka 1973 ambayo ilikuwa inavutana kuhusu umiliki wa eneo hilo ambapo baada ya majadiliano ilikubaliana kwa kauli mmoja kwamba mmliki halali wa eneo hilo ni Bibi Elizabeth Msalali.
Kutokana na Wilaya ya Manyoni kuonekana kuwa na migogoro ya ardhi kadhaa ya ardhi kwa muda mrefu sasa, mkakati maalum wa kusikiliza kero hizo umeandaliwa ambapo timu ya wataalam na viongozi wa Halmashauri hiyo unazungukia katika maeneo husika ili kuhakikisha migogoro yote inaisha kama ilivyoamriwa.
No comments: