WAZIRI LUKUVI AIFUMUA IDARA YA ARDHI HALMASHAURI YA WILAYA CHAMWINO.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amefanya ziara ya kushtukiza leo katika ofisi za ardhi za Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma ambapo ameagiza kubadilishwa vituo vya kazi Mkuu wa Idara ya Ardhi Bwana Letare Sinda na Afisa Mipango Miji Bwana David Msemo.

Waziri Lukuvi amefikia uamuzi huo baada kukagua utunzaji wa nyaraka pamoja na maombi ya vibali vya ujenzi yaliyowasilishwa kwenye ofisi ya Mipangomiji kwenye Halmashauri hiyo ambapo, alikerwa na ukiukwaji wa  sheria na miongozo ya kutoa vibali vya ujenzi na umilikishaji ardhi ambao umechangia malalamiko ya wananchi kuongezeka.

Lukuvi ameagiza Kamishna wa Ardhi na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Makao makuu ya Wizara watume wataalam wengine haraka iwezekanavyo ili wakasimamie uandaaji wa nyaraka za umiliki pamoja na utoaji vibali vya ujenzi katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Ameongeza kwamba, Wilaya ya Chamwino ndiyo Wilaya pekee ambayo ilipewa upendeleo na Wizara wa kupatiwa vifaa vya Upimaji, gari la Idara ya ardhi na vifa vya Kompyuta lakini ndiyo Wilaya inayolalamikiwa zaidi katika mkoa wa Dodoma.

‘Jiji la Dodoma linakua kwa haraka sana, Wilaya ya Chamwino ndiyo Wilaya namba moja na Ikulu ipo ndani yake. Ni lazima iwe wilaya ya mfano kwenye utoaji huduma za sekta ya ardhi.  Muda wa kufanya kazi kwa mazoea hakuna tena, kila mtaalam afuate miongozo iliyowekwa na Serikali ya kutolea huduma, Alisema Lukuvi’

Lukuvi Alisema, Wilaya ya Chamwino imekuwa na tamaa ya kuuza viwanja kwa gharama kubwa, kiasi cha kuwakatisha tamaa wananchi masikini na wanyonge ambao ndio wazawa wa Chamwino. Hali hii inapelekea wananchi kuyakimbia maeneo yao na kwenda kutafuta maeneo sehemu nyingine na kuanzisha Makazi holela.

Aliongeza kwamba, wananchi wachache wanaoweza kununua viwanja ndani ya Wilaya hiyo, bado wanakutana na changamoto nyingine ya gharama kubwa za vibali vya ujenzi ambapo hata kumbukumbu tuu za jumla ya maombi yaliyopokelewa na yaliyotolewa hakuna.

 Mbali na sheria na miongozo kutokufuatwa, Waziri Lukuvi amesema maombi mengi ya vibali vya ujenzi hayajatolewa na hakuna nyaraka yeyote inaoonesha sababu zilizokwamisha maombi hayo.

“Haiwezekani mwananchi alete maombi ya kibali cha ujenzi yeye mwenye na asikifuatilie kama taratibu za utoaji huduma ni rafiki na ziko wazi, Alisema waziri Lukuvi”.

Aidha, Mhe.Waziri amesema kufanya kazi kwa mazoea na kutokuzingatia sheria, taratibu na kanuni katika utoaji wa huduma kunatengeneza mianya ya rushwa na kuzalisha malalamiko ya wananchi.

Katika muongozo wa utoaji vibali vya ujenzi uliotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Rais TAMISEMI uliwataka wataalam wote wanaohusika kupitia maombi kuweka utaratibu wa kukutana wote kwa pamoja na kupitia maombi yaliyowasilishwa ili kutoa mwanya kwa kila mtaalam kujiridhisha na kipengele kinachomuhusu. Aidha muongozo huo uliwataka wataalam hao kuhakikisha kibali cha ujenzi kinatolewa ndani ya siku saba tangia maombi yalipowasilishwa.

No comments: