UBUNIFU UANDAAJI TAMASHA LA SARAKASI LAMKOSHA WAZIRI BASHUNGWA
Waziri wa Habari ,Sanaa,Utamaduni na Michezo Innocent Bashungwa(wa pili kushoto) pamoja na watazamaji wengine wa sanaa ya sarakasi wakishangilia burudani ya sarakasi iliyokuwa ikitolewa na wasanii wa sarakasi.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI wa Habari ,Sanaa,Utamaduni na Michezo Innocent Bashungwa amesema amefurahishwa na tamasha la sarakasi linafahamika kwa Sircus Mama Afrika linaoendelea Masaki jijini Dar es Salaam huku akitumia nafasi hiyo kuelezea mipango ya kukuza tasnia ya sanaa nchini.
Bashungwa akiwa katika tamashaa hilo ameshuhudia idadi kubwa ya raia wa kigeni ambao wamefika kutazama burudani ya sanaa za sarakasi zinazotolewa na vijana wa kitanzania ambapo amesisitiza Wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau walioandaa tamasha hilo kuona linafanyika katika miji mikubwa nchini.
Akizungumza wakati wa tamasha hilo la Sarakasi linaloendelea Masaki mwisho jijini Dar es Salaam, Waziri Bashungwa amesema ameshuhudia raia wa kigeni ambavyo wamekuwa wengi na hiyo inaoesha hiyo ni fursa kwa wasanii.
"Niwapongeze waandaaji wa Sircus Mama Afrika,tumefika hapa Waswahili ni sisi tu waliobakia wote ni watu kutoka mataifa mbalimbali,hii inamaanisha wateja wa sarakasi hizi wanachokipato cha kulipa kwa gharama yoyote ili mradi wanapata burudani.
"Kwa hiyo tunampongeza muaandaji wa Sircus Mama Afrika Constantine Magavila, hivyo kuna kila sababu ya kukaa na kuangalia namna gani Chuo chetu cha Sanaa Bagamoyo kinaweza kusaidiana na Circus mama Afrika tuaendelea kutoa burudani mbalimbali za aina hii.
"Ni ubunifu mzuri ambao umefanyika hapa, nimependezwa nao sana, lakini sisi kama Wizara na watendaji wetu tunapozungumzia kukuza sanaa basi ni kama hivi na ndio fursa kwa vijana wetu kuonesha vipaji walivyonavyo katika sanaa,"amesema.
Aidha amewapongeza wasanii wote wanaoshiriki katika kutoa burudani katika tamasha hilo ambalo sasa limeongezwa muda na litafanyika hadi Februari mwaka huu na hiyo inatokana na mapokeo makubwa ya watu wanaohudhuria Sircus Mama Afrika.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Sanaa Bagamooyo nchini(TASUBA),Dk.Habert Makoye amesema kupitia tamasha hilo la sarakasi mbali ya kuwapongeza waandaaji kuna mambo ya kujifunza na hasa ubunifu, ufundi na utalaamu uliotumika hadi kulifanya kuwa kubwa kwa kiwango hicho.
"Kuna mambo mengi ya kujifunza, tunaona watu wamejaa lakini kujaa kwao kunatokana na mipango imara ya waandaaji ambayo wameifanya , hivyo sisi Chuo cha Sanaa Bagamoyo tunao wajibu wa kujadiliana na hawa wenzetu kama sehemu ya kujifunza kutoka kwao na tutengeneze mshikamano,"amesema Dk.Makoye.
Wakati huo huo mmoja ya waratibu wa tamasha la Sircus Mama Afrika Constatine Magavila amesema tamasha hilo wamelifanya kwa kupata baraka zote kutoka Bodi ya Utalii Tanzania ambao ndio wameshirikiana nao.
Kuhusu tamasha hilo amesema kuwa lengo kuu ilikuwa ni kutengeneza mazingira ya burudani ambayo inakiwango cha kimataifa lakini vionjo vya kitanzania na hilo kwa maana pana linaweza kuhamasisha sio tu ushiriki wa watanzania kwa maana ya watanzania wa kawaida lakini hata wageni.
"Maana vivutio ni vingi ambavyo vinawahamasisha wageni kukaa na kuona tija kutembelea nchi mbalimbali za Afrika na hasa Tanzania.Ndio maana hata tulipofungua tamasha hili mgeni wetu wa heshima alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwasababu naye alitambua ukubwa wa matukio kama haya.
"Matukio kama haya yanawahamasisha sio tu watanzania bali hata watu wanaotoka nje, tunajua nyakati hizi za Corona kusafiri nje ya nchi ni vigumu hata kwa wale waliokuwa ndani ya nchi yetu, kwetu hapa hakuna Corona kutokaa na jitihada mbalimbali zilichokuliwa na Serikali yetu chini ya uongozi mahiri wa Rais wetu Dk.John Magufuli.
"Kwa kuwa nchi yetu haina Corona, tamasha hili la sarakasi ndio tamasha pekee kubwa la sarakasi linaloendelea kufanyika duniani kwa sasa, haliko mahali kokote zaidi ya hapa kwetu na hiyo inatokana na mataifa mengine kuendelea kusumbuliwa na Corona.
"Hivyo tumeongeza muda tulianza Desemba mwaka 2020 na sasa tumeogeza muda litaendelea hadi Februari mwaka huu,muitikio ni mkubwa, watu ni wengi wanaokuja kuangalia burudani hii ya sarakasi,"amesema Magavila.
No comments: