Tuache Maneno, Tufanye Kazi''DC Gondwe.
Hiyo ni kauli ya mkuu wa wilaya ya Temeke mheshimiwa Godwin Gondwe wakati akizungumza na viongozi pamoja na baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Sterio , alipotembelea soko hilo mapema leo,lengo likiwa ni kukagua hali ya usafi katika eneo lote la soko,pamoja na mitaa ya jirani na soko hilo.
Akiwa sokoni hapo Mhe. Gondwe amesema kwamba ametembea eneo lote la soko,ameona hali halisi ya usafi katika eneo hilo, viongozi pamoja na wafanya biashara wanajitahidi kufanya usafi katika maeneo yao,lakini kutokana na hali halisi iliyopo,bado iko haja ya kuwa na siku ya kufanya usafi kwa pamoja.
" Kwa yale niliyoyaona pale Mwenyekiti,mtaua watu.Tuache maneno,tufanye kazi.Ule utaratibu mlioniambia kwamba huwa mnafanya usafi kila siku jioni,endeleeni nao,kama kawaida,lakini ni lazima kuwa na siku ya usafi wa pamoja.Ule uchafu niliouona pale,ni kwa sababu hakuna muda wa pamoja wa kufanya usafi.
Ninyi viongozi nendeni mkakae na wafanyabiashara wenzenu wa soko hili mjadiliane,mpange muda wa usafi wa pamoja. Siku tuliyoipitisha kwa ajili ya usafi ni Jumamosi, na katika maeneo mengine,tumepanga muda wa kuanzia saa 12 mpaka saa 3 asubuhi.Lakini kutokana na asili ya hapa,hatutaki kuwaingilia,angalieni wenyewe ni muda gani utafaa,kubalianeni. Ninachotaka,ni usafi ufanyike.Uhai hauna mbadala ndugu zangu"
Aidha Mhe. Gondwe ameitaka idara ya Usafi wa Mazingira kwa kushirikiana na uongozi wa Kata, kusimamia suala la uzoaji taka katika eneo hilo, kwa kuhakikisha kwamba katika siku hiyo ya usafi wa pamoja, yanakuwepo magari ya kubeba taka ya kutosha ,ili taka zote zitakazokusanywa ziweze kuondolewa mara moja.
Mhe. Gondwe ameendelea kukagua usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Wilaya yake,ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira Kiwilaya,iliyofanyika mwezi Novemba 2020 katika eneo la Mbagala Rangi Tatu.
No comments: