TAKUKURU MANYARA YAANDAAA KONGAMANO LA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA KWA WENYE MAHITAJI MAALUM
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Joseph Mkirikiti akifungua warsha ya elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa makundi maalum Mjini Babati iliyotolewa na TAKUKURU.
Katibu wa Chavita Mkoa wa Manyara, Anna Ngalawa akizungumza kwenye warsha ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wenye mahitaji maalum iliyoandaliwa na TAKUKURU .
………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Manyara
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imeandaa kongamano la mapambano dhidi ya rushwa kwa wenye mahitaji maalum.
Katika kongamano hilo pia, wawezeshaji kutoka mfuko wa Bima ya Taifa ya Afya NHIF wametoa elimu juu ya Bima ya afya kwa kuwa suala la afya na tiba ni mtambuka kwa jamii ya wenye mahitaji maalum.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo mjini Babati kwenye kongamano hilo lililoshirikisha kundi la wenye mahitaji maalum. Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Serikali jumuishi kwa makundi yote na imekuwa ikiwajali raia wake bila ubaguzi ikiwemo kundi lenye mahitaji maalum ikiwemo kujadili changamoto zinazowahusu ikiwemo kero ya rushwa.
Amesema kupitia kongamano hilo wataibuka kina Amina Mollel aliyekuwa mbunge wa viti maalumu aliyeibua hoja ya walemavu kupata mikopo isiyo na riba ya asilimia mbili kupitia mapato ya ndani ya kila Halmashauri.
“Tunafahamu pia changamoto ya baadhi ya Halmashauri zinazokwamisha kundi hili kushiriki makongamano mbalimbali hasa yanayoweza kuleta matokeo chanya kwa walemavu kama siku ya wenye ulemavu duniani kwa kutotoa fedha za kuwasafirisha, kwenye mkoa wa Manyara hili lipo ndani ya uwezo wako mheshimiwa Mkuu wa mkoa,” amesema Makungu.
Amesema jamii ya wenye uhitaji maalum imekuwa ikilalamikia kupunguziwa kodi katika vifaa wezeshi ili waweze kuvipata kwa bei nafuu na hilo ni suala la kisera ambapo Wana imani kuwa litafikiwa kwa ngazi husika kwa faida ya kundi la wenye mahitaji maalum. Mkuu wa mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti amezitaka taasisi za Serikali na za binafsi kuwa na wataalamu wa lugha za alama ili kuwezeshwa wasio na uwezo wa kusikia wapate mawasiliano maeneo mbalimbali. Mkirikiti amesema endapo kungekuwa na wataalamu wa lugha za alama kila maeneo ya Taasisi hizo wenye ulemavu wa kusikia wataondokana na changamoto ya kutopata baadhi ya haki wanazostahili kupata.
Hata hivyo, amewapongeza viongozi wa wilaya za mkoa huo kwa kutekeleza ukopeshaji wa kundi la wavemavu kupitia mapato ya ndani. Amesema kutokana na uaminifu na urejejeshwaji wa mikopo unaofanywa na kundi la walemavu, halmashauri zitoe kipaumbele kwao ili waweze kunufaika zaidi.
Katibu wa chama cha viziwi Tanzania (Chakiwata) Mkoani Manyara, Anna Ngalawa amesema rushwa ni tatizo kubwa na la muda mrefu katika nchi zote duniani na baadhi ya wanasiasa hutumia wakati wa uchaguzi ili kuingia madarakani.
Ngalawa amesema athari za rushwa kwa jamii husababisha upendeleo kwa wale walio na uwezo katika kupata huduma na kusababisha kukosekana haki katika jamii. Amesema husababisha wananchi kutokuwa na imani na Serikali yao kwa kushindwa kutoa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji na kusababisha mifarakano kwa jamii viongozi wanaposhindwa kutenda haki kutokana na rushwa.
“Huhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi mfano rushwa katika siasa, husababisha vifo mfano kukosa matibabu kwa kushindwa kutoa hongo na husababisha kupindishwa sheria, kanuni na taratibu.
Amesema rushwa ni dhambi kwa mujibu wa dini kwani katika Biblia kutoka 23:8 hupofusha macho hao waonao na kuyapotoa maneno ya wenye haki na Qur’an sura ya 4 aya ya 135 ni dhuluma ambayo ni kinyume cha uadilifu.
No comments: