NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA MHE.NDEJEMBI APONGEZA MCHANGO WA TASAF KATIKA KUPAMBANA NA UMASKINI NCHINI


Na Estom Sanga- Dodoma 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF umeendelea kuwa kichocheo muhimu katika kupiga vita umaskini nchini na hivyo kuutaka Uongozi wa Mfuko huo kuboresha zaidi huduma zake ili ziwafikie wananchi wanaozihitaji kwa ufanisi zaidi. 

Mhe.Ndejembi amesema kutokana na mchango wake muhimu katika kupiga vita dhidi ya umaskini , Serikali imeendelea kuuamini Mfuko huo na kuupa fursa ya kupata fedha ili uweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi. 

Ametoa rai hiyo mjini Dodoma alipotembelea ofisi za TASAF na kukutana na Watumishi wa Mfuko huo walioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake , Ladislaus Mwamanga akiwa katika ziara ya kujitambulisha na kuona utendaji kazi wa taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Magufuli mwanzoni mwa mwezi uliopita. 

Aidha Mhe. Ndejembi ameuagiza Uongozi wa TASAF kufanya tathmini za huduma zitolewazo na mfuko huo mara kwa mara ili kujiridhisha ikiwa Walengwa wake wanatumia vizuri fursa zitolewazo na pale inapobainika kuwa Walengwa wanakiuka misingi ya kuanzishwa kwake hatua madhubuti zichukuliwe mara moja. 

Akitoa taarifa ya utendaji kazi, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga ameeleza namna Mfuko huo ulivyosaidia jitihada za Serikali za kuwahudumia wananchi hususani wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri . Amesema kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Walengwa wamefanikiwa kuboresha makazi yao, kusomesha watoto , kupata huduma za Afya kwa uhakika baada ya kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii,kuanzisha miradi ya kiuchumi na kujiongezea kipato. 

Bwana Mwamanga pia amesema kuanzia mwaka huu TASAF itaanza kutekeleza maagizo ya Rais Mhe. Dr. John Pombe Magufuli ya kuwafikia wananchi watakaokidhi vigezo vya umaskini uliokithiri katika mitaa, vijiji na shehia kote nchini. 

Adha Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF ameishukuru Serikali kwa kuuwezesha Mfuko huo kupata fedha za ndani na Wafadhili jambo ambalo amesema limeupa nguvu zaidi ya kuwafikia Walengwa nchini kote kwa wakati na kuwa sekta za elimu, afya na maji pia zitapewa msukumo katika utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF. 

Kuhusu uhakiki wa Walengwa Mwamanga amesema suala hilo ni endelevu na limekuwa likitekelezwa kila baada ya miezi miwili ili kuondoa uwezekano wa kunufaisha watu ambao hawajakidhi vigezo vya Mpango.
‘’Karibu kwetu Mhe.Naibu Waziri Deogratus Ndejembi’’…. hivi ndivyo Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus mwamanga anavyomkaribisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alipotembelea ofisi za Mfuko huo mjini Dodoma.
Picha ya juu na chini Mhe. Ndejembi akiwa katika picha na baadhi ya Watumishi wa TASAF mjini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi za Mfuko huo.



No comments: