WAZIRI UJENZI ATINGA OFISINI, AWAONYA WANAOFANYA KAZI KWA MAZOEA


SIKU moja baada ya kuapishwa na Rais Dk John Magufuli Ikulu Chamwino, Dodoma, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuliho na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Godfrey Msongwe wameripoti katika ofisi za wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma na kupokekewa na Menejimenti ya Wizara hiyo.

Wakizungumza na Menejimenti hiyo baada ya kufika ofisini hapo wote kwa pamoja wameomba ushirikiano kutoka kwa Watumishi wote huku wakisisitiza weledi na kujituma kwenye kazi kwa kila mmoja.

Akizungumza katika kikao kifupi na watendaji hao, Waziri Dk Leonard Chamuliho amewataka watumishi wote wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kufanya kazi kwa kutumia taaluma zao na kwamba hawatomvumilia mtumishi yoyote ambaye ataenda kinyume na matarajio waliyojiwekea.

" Tunashukuru kwa mapokezi yenu yaliyojaa upendo, Wizara yetu inaongoza taasisi 25 ambapo 10 kati yao zipo wajenzi na 15 zipo chini ya sekta ya uchukuzi na zote zinaratibiwa na wizara yetu kupitia Idara zake mbalimbali niwatake wakuu wote wa Idara zinazosimamia taasisi hizo kuhakikisha zinaleta tija kwa Taifa letu na watanzania kwa ujumla.

Rais Dk Magufuli jana alichambua wizara zote na yetu ikapigiwa makofi na hiyo ni kwa sababu ilibebwa na baadhi ya taasisi sasa zile taasisi ambazo hazikutajwa pale lengo zetu ni zipige hatua hivyo tutapeana maelekezo mahususi ili tuweze kupiga hatua kwa pamoja," Amesema Dk Chamuliho.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Mhandisi Godfrey Msongwe amewaomba watumishi wote wa wizara hiyo kumpa ushirikiano kwa kuwa yeye ni mgeni ndani ya wizara hiyo huku akiwaahidi kuwa atajifunza kwa haraka ili aweze kwenda na spidi inayotakiwa na Rais Magufuli.

" Niwaombe tushirikiane kama Timu ili tuweze kufika tunapopataka, kwenye sekta zetu hizi yapo mambo ambayo yaliahidiwa na Rais wakati wa kuomba kura na yapo kwenye Ilani ya CCM, ni kazi yetu kwenda kuyasimamia na kuyatekeleza kama yalivyoelekezwa.

Wizara yetu ni wizara yenye taasisi kila mahali mfano Tanroad na Tamesa ambao wako nchi nzima, twendeni huko tukikaa ofisini na kusubiri mafaili tutamkwamisha Rais wetu, kila mmoja atoke akashughulike na eneo lake," Amesema Mhandisi Msongwe.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuliho akizungumza na Menejimenti na wakuu wa Idara kutoka wizarani hapo baada ya kuwasili leo asubuhi.
 Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Msongwe akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa Wizara hiyo leo jijini Dodoma.

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuliho akiwasilia katika ofisi za Wizara hiyo katika mji wa kiserikali Mtumba jijini Dodoma na kupokelewa na Menejimenti ya Wizara hiyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Msongwe akiwasili katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma na kupokelewa na Menejimenti ya Wizara hiyo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,   Dk Leonard Chamuliho na Naibu Wake, Mhandisi Godfrey Msongwe wakikabidhiwa zawadi ya Maua kutoka kwa Menejimenti na Watumishi wa Wizara hiyo baada ya kuwasili ofisini hapo Mtumba jijini Dodoma leo.

 

No comments: