WAZIRI AWESU AANZA KAZI KWA KISHINDO, AMTUMBUA MKURUGENZI WA DUWASA DODOMA
KUMEKUCHA! Saa 24 baada ya kuapishwa na Rais Dk John Magufuli kuwa Waziri wa Maji, Jumaa Awesu ameanza kazi kwa kishindo baada ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Pallangyo.
Waziri Awesu ametoa maamuzi hayo leo jijini Dodoma alipokutana na kufanya kikao cha pamoja na viongozi Wizara hiyo, viongozi wa Duwasa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo huku akiwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Akizungumza katika kikao hicho, Awesu amesema pamoja na Mhandisi Pallangyo kufanya kazi kwa muda mrefu na weledi bado Mkoa wa Dodoma unamhitaji mtu mwingine ambaye anaweza kukimbia na kasi iliyopo na kumaliza changamoto ya maji ambayo imekua ikiwakabili wananchi wa mkoa huo.
Waziri Awesu amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Anthony Sanga kumshauri na kumletea kwa haraka mtu ambaye atakuja kuchukua nafasi hiyo ya Pallangyo na kwamba Mhandisi huyo atapangiwa kazi nyingine.
" Naheshimu kazi kubwa iliyofanywa na Mhandisi Pallangyo, lakini ninahitaji mtu mwingine hapa Dodoma na wewe tutakupangia kwingine, niwatake watendaji na watumishi wote mlio chini ya Wizara ya Maji kuacha ufanyaji kazi wa mazoea na mtumie taaluma zenu kuondoa kero na changamoto ya Maji, Sisi hatujaajiri vibaka tumeajiri wataalamu, tunataka kuona mkitumia utaalamu wenu kwa weledi.
Msichukulie watu kukosa maji kuwa ni mazoea, haiwezekani kwangu na kwenu maji yanatoka halafu wananchi hawana maji huko ni kutengeneza chuki, mtu ambaye yupo hapa kwa ajili ya kulakula nimhakikishie hapa hapati kitu, tutamuondoa na hata kama ana mapembe tutayashusha," Amesema Awesu.
Kwa upande wake Mhandisi Pallangyo amempongeza Waziri Awesu kwa kuteuliwa na kuaminiwa na Rais na kuhakikishia kuwa amepokea maamuzi hayo kwa utii na kwamba atakua tayari kutumwa popote ambapo itaonekana anafaa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Anthony Sanga akizungumza katika mkutano wa pamoja na Waziri wa Maji, Jumaa Awesu leo jijini Dodoma. Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Maji na Duwasa wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Awesu alipofanya kikao kazi nao leo asubuhi jijini Dodoma.
No comments: